Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yawaasa wahariri wa vyombo vya habari kutumia kalamu kulinda amani ya taifa
Na. Noel Rukanuga, DODOMA
Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini
kutumia kalamu zao kwa uadilifu, kwa kuzingatia maadili ya taaluma na
kuhakikisha wanahabarisha umma kwa namna inayolinda amani na usalama wa taifa.
Akizungumza wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kati ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari, kilichofanyika leo Septemba 12, 2025 katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali, jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Ipyana Mlilo, amesema kuwa sekta ya habari ni mhimili muhimu katika maendeleo ya taifa, hivyo kikao kazi hicho kimetoa nafasi ya kuimarisha ushirikiano baina ya wahariri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ili kuendelea kutoa elimu ya kisheria kwa jamii kwa weledi.
“Kikao
hiki kimekuwa na manufaa makubwa katika kuhakikisha jamii inapata uelewa mpana
kuhusu masuala ya kisheria. Tumejadiliana mambo mengi muhimu ambayo
yatashughulikiwa kwa lengo la kuelimisha na kulinda maslahi ya umma,” alisema
Mlilo.
Alisisitiza
umuhimu wa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili
ya taaluma na kuhakikisha wanachangia katika ustawi na usalama wa taifa.
Akiwasilisha
taarifa ya majukumu ya Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), Rais wa
Chama hicho Bavoo Junus, amesema kuwa kuwa TPBA ni Chama muhimu katika
kusimamia, kulinda na kutetea maslahi ya Serikali na rasilimali zake.
Alibainisha
kuwa TPBA ni chama cha kitaaluma kinachowaunganisha wanasheria wote wanaohudumu
katika taasisi za umma ikiwemo Wizara, Halmashauri, Wakala, na Mashirika ya
umma pamoja na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa.
“Kupitia
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, TPBA imefanikiwa kueneza elimu ya
sheria kwa wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Junus.
Aliongeza
kuwa TPBA limeanzisha jukwaa la mawakili wa serikali kwa ajili ya kubadilishana
uzoefu kitaaluma, kujadili changamoto, na kuweka mikakati ya pamoja ya kutetea
maslahi ya Serikali.
Pia
alieleza kuwa chama hicho hutoa mafunzo endelevu kwa wanachama wake ili
kuongeza uelewa na ufanisi wa kiutendaji, badala ya kutegemea waajiri pekee.
Junus
alieleza kuwa TPBA ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 16A (1) cha Sheria ya
Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268,
pamoja na Tangazo la Serikali Na. 589 la tarehe 16 Agosti 2019.
Aidha,
alifafanua kuwa TPBA ni tofauti na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),
ambapo TPBA uwakilisha wanasheria wa Serikali, wakati TLS hujumuisha wanasheria
wote nchini, bila kujali mwajiri.
Alisema
kuwa chama wa TPBA unategemea ajira ya mwanachama katika utumishi wa umma,
wakati TLS huruhusu wanachama wake kuendelea hata baada ya kutoka kazini.
Akizungumza
kwa niaba ya wahariri walioshiriki kikao kazi hicho, Mhariri Mkuu wa Clouds
Media, Joyce Shebe, alipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
kuratibu kikao hicho ambacho kimetoa maarifa na uelewa kuhusu masuala ya
kisheria kwa wahariri, jambo litakalosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu
yao.
“Tunathamini
nafasi hii ya kushirikishwa katika kujadili masuala ya sheria ambayo ni msingi
wa kazi zetu. Tunatarajia ushirikiano huu uendelee,” alisema Shebe.
Chanzo:
Fullshangwe Blog
Comments
Post a Comment