Madereva wa Serikali wahimizwa kuendesha kwa ustadi, kulinda Usalama barabarani
Na. Sizah Kangalawe, DODOMA
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amewahimiza madereva wa Serikali kutumia
vyema mafunzo waliyopatiwa katika kuboresha utendaji kazi wao na kuleta tija
zaidi.
Alitoa maagizo hayo Septemba 04, 2025 jijini Dodoma wakati akifunga Kongamano la Nne la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST) lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
"Naamini
mada mlizofundishwa hapa zitakwenda kuboresha uwezo wenu katika utendaji kazi
na kuleta tija zaidi katika kuhakikisha mwajiri mkuu ananufaika na mafunzo
mliyopata kupitia kongamano hili, na ninaamini kuwa kushiriki kwenu kutapelekea
kuendesha magari kwa ustadi na kupunguza matukio ya ajali. Tutajua thamani ya
abiria mliowabeba na kuendesha tukiwa tunawakinga na madhara, lakini pia mtajua
thamani ya vitu mnavyobeba kupitia magari hayo ambayo mnatakiwa mvisafirishe
kwa usalama,” alisema Senyamule.
Alifafanua
kuwa madereva wa Serikali ni mhimili muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya
kila siku ya Serikali kwani ndio wanaohakikisha usafiri wa viongozi na
watumishi unakuwa salama, wenye ufanisi na unaoendana na hadhi ya Taifa la
Tanzania.
Kwa
upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, alisema
Serikali imeboresha muundo mpya wa madereva ambao pia unasimamia maboresho ya
mishahara na stahiki nyingine kwa madereva wa Tanzania Bara.
Kongamano
hilo lililoandaliwa na CMST, limefanyika kwa siku tano ambapo lilianza Agosti
31 na limetamatika Septemba 04, 2025 huku likienda sambamba na kaulimbiu
"Dereva wa Serikali, epuka ajali, linda gari lako na watumiaji wengine wa
barabara, shiriki uchaguzi mkuu Oktoba 2025."
Chama
cha Madereva wa Serikali kilianzishwa mwaka 2013 na kusajiliwa Wizara ya
Mambo ya Ndani mwaka 2015 kwa Na. ya Usajili S.A. 20314, ambapo hadi sasa kina
jumla ya wanachama zaidi ya 3,500.
Comments
Post a Comment