ACC yatoa vifaa vya Mil. 62 kwa watoto wenye changamoto ya Afya
Na. Sofia Remmi, DODOMA
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amepokea na kukabidhi vifaa vya
michezo, vya kujifunzia pamoja na vitendea kazi vya watoa huduma za afya ngazi
ya Jamii ili viweze kuwafikia walengwa waliopo katika baadhi ya halmashauri za mkoa
huu.
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jengo la Mkapa.
Akizungumza
na baadhi ya wadau na watoa huduma ngazi ya jamii amesema Mkoa unashirikiana na
Shirika la Action for Community Care (ACC) katika kutekeleza miradi ya Imarisha
Afya na ViiV Pediatric Breakthrough Partnership ambayo inalenga kusaidia watoto
na vijana wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wenye umri wa miaka 0-19. Miradi
inawezesha kuwaibua na kuwaunganisha watoto na vijana kwenye matibabu,
kuwasaidia kubaki katika huduma na matibabu na kuishi maisha yenye afya.
“Vifaa
vya michezo na vya kujifunzia vinavyopokelewa leo vina umuhimu wa kipekee
kwa kuwa vitawezesha uchangamshi na ukuaji wa ubongo wa watoto na
kuwamotisha watoto na vijana kuhudhuria kliniki kwa ajili ya huduma za VVU na
kupunguza utoro na kuamasisha watoto dhidi ya kujifunza zitaongeza hamasa kwa
wazazi na walezi kuwaleta watoto kwenye vituo vya tiba na matunzo hivyo, wakati
wakisubiri huduma watoto na vijana watajifunza baadhi ya mambo badala ya kukaa
bila kufanya kitu” alisema Senyamule.
Miradi
hii ililenga pia kuwatambua na kutoa mafunzo kwa Wakunga wa Jadi kwa lengo la
kuwaelekeza kuhusu umuhimu wa kuwaelimisha wajawazito kujifungulia katika vituo
vya kutolea huduma za afya kwa usalama wao na watoto watakaozaliwa.
Kwa
upande wake Meneja wa Miradi, Merina Mgongo alisema ACC ni shirika lisilo la
Kiserikali na linatekeleza shughuli zake katika Halmashauri nne za Mkoa wa
Dodoma ikiwemo Kongwa, Chamwino, Mpwapwa na Dodoma Mjini.
“ACC
inateleza miradi ya Afya, Elimu, Kuboresha vifaa vya michezo Kama Bembea za
watoto, mipira ya miguu na mkono, kikapu, kamba za kuruka, midoli, vinanda,
runinga na vinginevyokuimarisha katika ngazi ya jamii na mazingira” alisema
Mgongo.
Comments
Post a Comment