Miaka minne ya Dkt. Samia, Kizota yanufaika mikopo ya asilimia 10
Na. Coletha Charles, KIZOTA
Wananchi wa Kata ya
Kizota Halmashauri ya Jiji la Dodoma, waeleza kunufaika na mikopo ya asilimia
10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana, na watu wenye
ulemavu, ikiwa ni hatua ya kuinua maisha yao
kiuchumi na kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali.
Walieleza hisia zao mbele ya waandishi wa habari waliofanya ‘media tour’ kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika Kata ya Kizota kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Akizungumzia hali ya
mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kizota, Theresia Ntui alisema
kuwa tangu kuanza kwa utolewaji mikopo ya asilimia 10 katika serikali ya awamu
ya sita, Kata ya Kizota imenufaika kwa jumla ya shilingi 410,000,000 zilizotolewa
kwa vikundi mbalimbali vya kijamii.
Alisema kuwa katika fedha
hizo, vikundi 28 vya wanawake vilipokea shilingi 192,000,000 vikundi 16 vya
vijana vilipewa 164,000,000 na vikundi vitano vya watu wenye ulemavu walipata shilingi
49,000,000. “Mikopo hii ni yenye masharti nafuu, haina riba, na inatolewa kwa
mtindo wa kikundi. Vikundi hupatiwa muda wa ‘grace period’ inakuwa ni miezi
mitatu, ikipita hiyo miezi wanaanza kurejesha mkopo baada ya kutekeleza mradi
waliokuwa wanautaka na kikundi kama kikikopa milioni 10 kitarudisha milioni 10”
alisema Ntui.
Nae, Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Manyema, Jackson Samwel,
alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa vijana katika kujikwamua
kimaisha, na mafanikio ya kikundi chao ni ushahidi tosha kuwa serikali ya awamu
ya sita inatekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuwawezesha vijana.
Alisema kuwa mikopo hiyo imewatoa vijana wa kikundi hicho kutoka hali ya utegemezi na kuwa wajasiriamali, ambapo kikundi hicho kina jumla ya wanachama watano wanajihusisha na shughuli za usafirishaji. “Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa serikali, mbunge wetu na diwani kwa namna walivyotusaidia kupata elimu ya mikopo na hadi kufanikiwa kupata mkopo huu wa milioni sita. Tumenunua bajaji tatu na pikipiki mbili (bodaboda) na hadi sasa tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kuendesha shughuli zetu vizuri na kujitegemea kiuchumi” alishukuru Samweli.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Angel kutoka Mtaa wa Relini, Kata ya Kizota, Edina Mwanjila, alisema kuwa mkopo wa asilimia 10 ni mkopo usio na riba na ambao umekuwa msaada mkubwa katika kuboresha maisha ya wanawake kiuchumi, na kusaidia upatikanaji wa mahitaji ya familia.
Alisema kuwa
kikundi kinajihusisha na shughuli za ushonaji wa nguo (ufundi cherehani) ambapo
awali walikuwa na changamoto nyingi za kifedha na vifaa. “Baada ya kupata
taarifa kutoka kwa afisa maendeleo wa kata kuhusu mikopo ya asilimia 10,
tulielekezwa hatua za kuchukua na tukafuata taratibu, tukaanzisha kikundi,
tukasajiliwa rasmi, na hatimaye tukaomba mkopo wa shilingi milioni tatu tukiwa wanachama
watano. Kupitia mkopo huo, Angel Group tumenunua mashine ya kushonea ya
‘overlock’ kwa ajili ya kukamilisha ushonaji wa nguo ‘finishing’, pamoja na vifaa
vingine vya ushonaji” alisema Mwanjila.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan mikopo ya asilimia 10 imeendelea kuwa mkombozi kwa wananchi wa Kata ya Kizota huku wanufaika wakubwa wakiwa ni makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Fursa ya kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya ujasiriamali imekua kichocheo cha maendeleo katika Jiji la Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment