Kata ya Kizota yajivunia maendeleo makubwa ya miradi

Na. Asteria Frank, DODOMA

Diwani wa Kata ya Kizota, Jamal Ngallya afurahia mafanikio ya serikali kwa kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Kituo cha Afya, Shule ya Msingi Mahungu na stendi ya mabasi katika kata yake.




Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo kujionea miradi iliyotekelezwa na serikali katika Kata ya Kizota.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, kata hiyo imeshuhudia maendeleo makubwa. “Mimi leo naweza kuzungumza kuwa Kizota ya sasa hivi na ya miaka 10 nyuma ni vitu viwili tofauti, wakati mimi nazaliwa tulikuwa tunapata huduma za afya Makole na taasisi ya Magereza Isanga lakini leo Kizota tunatamba tumepata kituo cha afya kikubwa ambacho kinagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi 500,000,000 ambapo kwa Dodoma sasa hivi kituo hicho kitashika nafasi ya tatu kwa ukubwa na hivi karibuni kitaenda kufunguliwa ili kitoe huduma mbalimbali kwa wananchi” alisema Ngallya.

Aliongeza kuwa serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya mabasi ambayo itahudumia wananchi wengi.

“Ila pia mama ametoa bilioni sita kwaajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ambayo itakuwa stedi ya pili kwa ukubwa baada ya stendi ya Nanenane. Stendi hiyo pia itahudumia magari yanayotoka ukanda wa magharibi kama Kigoma, Musoma na Tabora. Stendi hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mabasi zaidi ya 200 na mkandarasi alishasaini mkataba wa ujenzi wa stendi hiyo” aliongeza Ngallya.

Nae Afisa Mtendaji wa Kata ya Kizota, Aidan Libenanga alisema kuwa suala la utawala bora linafanyika kwa uthabiti. Migogoro ya ardhi imepungua sana kutokana na mkakati wa kuitatua kufanikiwa.



Akiongelea suala la lishe, alisema kuwa kata imekuwa ikiadhimisha maadhimisho ya siku ya afya na lishe kila baada ya robo mwaka kwa mitaa yote. “Kwa upande wa lishe bora huwa tunaadhimisha kwa ngazi za mitaa kila baada ya robo mwaka kwa kuwashirikisha jamii inayotuzunguka kwa kuwapa elimu ya lishe. Tumekuwa tukiwashirikisha wataalam wa afya kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa vitendo ili wananchi waweze kuona na kuelewa kwa urahisi” alisema Libenanga.

Katika hatua nyingine Mkazi wa Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota, Steven Kapangala alishukuru mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kuwapelekea miradi mikubwa ya maendeleo kama stendi ya mabasi kwa sababu itasaidia kufungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali. “Lengo kubwa la serikali ni kutusaidia zaidi kuboresha mazingira ya kufanya biashara katika mazingira rafiki yenye kufikika na yenye tija lakini mradi huu wa wa stendi utatuletea maendeleo makubwa sana hasa katika mkoa wetu wa Dodoma” alisema Kapangala.




Kwa upande mwingine mkazi wa Kata ya Kizota, Rachel John, aliishukuru serikali kwa kusikia kilio chao cha kutaka stendi ya Kizota iboreshwe. “Mradi utakapoanza tutakuwa na fursa ya kufanya biashara na tutapata maendeleo kwa hakika tutafanya mambo mazuri. Mimi kama mama lishe naamini nitaweza kufanya sana biashara” alisema John.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri