Rais Samia aboresha huduma ya Maji Matumbulu
Na. Emanuel Charles, MATUMBULU
DIWANI
wa Kata ya Matumbulu, Emmanuel Chibago ameipongeza serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya sekta
ya afya, elimu, ujenzi wa ofisi ya kata pamoja na mradi wa maji ambao mpaka
sasa serikali imefanikiwa kujenga visima 12 vinavyotoa huduma ya maji kwa
wananchi wa kata hiyo.
Akiongelea
mafanikio ya serikali katika kipindi cha miaka minne kwa waandishi wa habari waliotembelea
miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2021 hadi sasa katika Kata ya
Matumbulu, Diwani Chibago alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kupeleka miradi
ya maendeleo katani hapo. Alisema kuwa serikali imechimba visima 12 vya maji ukilinganisha
na awali kilikuwepo kisima kimoja tu kikihudumia kata nzima. “Nipende
kuipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu mpaka sasa
katika Kata ya Matumbulu wananchi hawahangaiki na maji tena tofauti na hapo
mwanzo palikuwa na kisima kimoja cha maji ambacho kilikuwa ni tegemeo kwa
wananchi wote wa Kata ya Matumbulu” alisema Chibago.
Nae
Coletha Kapinga, Mtaalamu kutoka RUWASA na Mhasibu wa mradi wa maji Kata ya
Matumbulu alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi mkubwa wa maji ambao unahudumia mitaa mitatu ya
Kawawa, Nyerere na Mwongozo. “Mradi huu ni mkubwa, licha ya ukubwa wake unahudumia
idadi ya watu 4,120 ambao wananufaika na maji haya. Hizi zote ni jitihada za
Rais wetu kutuletea mradi huu uliogharimu shilingi 360,000,000. Tunamshukuru sana,
baada ya kupata mradi huu wananchi wanapata maji safi na salama” alisema
Kapinga
Kwa
upande mwingine Amosi Chipanyanga, ambae ni mkazi wa Mtaa wa Mpunguzi ‘A’, Kata
ya Matumbulu alimshukuru Rais kwa kuwapelekea mradi wa maji ambapo wakati wa
nyuma walikuwa wanahangaika kwa uhaba wa maji. “Tunashukuru kuletewa mradi huu
na Rais, Samia Suluhu Hassan kwasababu tulikuwa tunapata shida sana wakati wa
nyuma, lakini kwasasa tumepata manufaa makubwa sana kutokana na mradi huu watu
wanapata huduma kwa wakati muafaka” alimalizia Chipanyanga.
MWISHO
Comments
Post a Comment