Shule ya kwanza ya Sekondari yajengwa Matumbulu tangu Uhuru
Na. Nancy Kivuyo, MATUMBULU
Diwani
wa Kata ya Matumbulu, Emmanuel Chibago aishukuru serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu katani hapo.
Diwani wa Kata ya Matumbulu, Emmanuel Chibago, akitoa shukrani kwa rais |
Alitoa shukrani hizo wakati alipokuwa mwenyeji wa waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 katika Kata ya Matumbulu.
Chibago
alisema kuwa ni historia kwa Kata ya Matumbulu kuwa na shule ya sekondari na
kusema kuwa haijawahi kutokea tangu kupatikana kwa uhuru. “Kiukweli, nampongeza
sana Rais wetu pamoja na Mbunge Mavunde, wamehakikisha wananchi tunaoishi hadi
pembezoni mwa mji tunapata shule ili watoto wetu wapate elimu nzuri. Ukitazama
ndugu mwandishi, haya majengo ni ya kisasa kabisa, wanafunzi watasoma katika
mazingira mazuri na italeta chachu ya ufaulu kwasababu kule msingi walipo sasa
hivi watasoma kwa bidii ili wafaulu waje sekondari” alisema Chibago.
“Serikali
yetu ni sikivu, tuliomba tujengewe shule hapa na tumeletewa kiasi cha shilingi 544,000,000
kupitia mradi wa SEQUIP, ndio matunda yake haya tunaiona shule ipo mbioni
kukamilika. Tuna kila sababu ya kujivunia sekondari hii na tutaitunza kwa namna
ya kipekee kuhakikisha kwamba inafaa kwa vizazi vyetu na hata vya baadae”
alisisitiza Chibago.
Nae
Afisa Elimu Kata ya Matumbulu, Ally Mgoo aliishukuru serikali kwa kujenga shule
katani hapo kwasababu itasaidia wanafunzi waliokua wanaenda kata jirani kusoma
kubaki hapo na kupata elimu. “Serikali yetu kupitia rais, mbunge na diwani
wamefanya jambo la msingi kuipa kipaumbele sekta ya elimu katika kata yetu.
Watoto walikua wanatembea mbali kwenda kusoma, kuna ambao walikatiza masomo
sababu ya umbali, wapo waliokumbana na vishawishi wakapata mimba na kuacha
masomo. Hivyo, ujio wa shule hii utaboresha elimu katika eneo hili na
tunategemea kupata wasomi wengi” alishukuru Mgoo.
Katika
hatua nyingine Vicent Yohana aliipongeza serikali kwa kufanya maboresho katika
sekta ya elimu na kuiwezesha kata kupata shule ya sekondari. “kwakweli,
tunaipongeza serikali kwa kutuletea maendeleo katika elimu, watoto wetu sasa
watasoma katika mazingira mazuri na ninaamini watafaulu. Hii shule ni mfano
mzuri wa maendeleo mengine katika kata yetu. Tunashukuru sana kwa hili” alishukuru
Yohana.
MWISHO
Comments
Post a Comment