Mradi wa Maji ya Mvua uliofadhiliwa na TASAF wasaidia wanafunzi Shule ya Msingi Ipala
Na. Emanuel Charles, IPALA
Mwenyekiti
wa Kamati ya TASAF Taifa, Peter Ilomo ameupongeza uongozi wa Kata ya Ipala kwa
kuendelea kutunza miradi iliyofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ukiwemo
mradi wa ukusanyaji maji ya mvua unaopatikana katika Shule ya Sekondari Ipala wenye
lengo la kuondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa wanafunzi shuleni hapo.
Akizungumza
katika ziara ya kukagua miradi iliyotekelezwa na TASAF, Ilomo alisema kuwa lengo
la kwenda kukagua mradi huo ni kuangalia kama unafanya kazi na kusaidia wanafunzi
kama ilivyokusudiwa. “Tunashukuru mradi ulianza 2022 na kumalizika 2023,
kwakuwa tayari mradi umeshakamilika na jamii inayozunguka mradi huu kwa maana
ya wanafunzi na waalimu wananufaika tunasema asante sana. Lengo lakuja hapa ni
kukagua kama mradi unafanya kazi kwasababu mara nyingi miradi unaweza
kukamilika lakini usifanye kazi, nipongeze uongozi wa hapa Ipala, ninyi mmekuwa
wa tofauti” alisema Ilomo.
Pia
aliongeza kwa kusema kuwa uongozi wa Kata ya Ipala unapaswa kuendelea
kufuatilia kwa ukaribu changamoto za wanufaika wa TASAF na kuwasaidia kutatua
changamoto zao. “Kama kuna mnufaika ana changamoto awasilishe ili aweze
kutatuliwa. Lakini pia viongozi fuatilieni kwa makini kwasababu kuna baadhi ya
wazee hawasemi. Tumebakiza miezi tisa ili kumaliza mwaka, miezi hii si mingi. Hivyo,
basi fedha mtakazo zipata katika kipindi hiki cha miezi tisa zitumike vizuri”
aliongeza Ilomo.
Nae mmoja wa
wanufaika wa TASAF, Christina Fande aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuleta mpango huo kwasababu umeweza kumsaidia kununua ng’ombe wa kulimia, jembe
la kulimia pamoja na ujenzi wa nyumba ya kuishi. “Katika mpango huu wa kunusuru
watu masikini nilianza kupokea shilingi 40,000 ambayo nilikuwa naiwekeza sehemu
na baadae nikaweza kununua ng’ombe wa kulima, jembe la kulimia pamoja na ujenzi
wa nyumba yenye vyumba vitatu na sebule. Nawaasa wenzangu ambao ni wanufaika wa
TASAF, watumie vizuri fedha wanazopata ili kuweza kufanya maendeleo” alisema
Fande.
MWISHO
Comments
Post a Comment