WAAJIRI DODOMA WATAKIWA KUSAIDIA WANAWAKE KUNYONYESHA WATOTO MAZIWA YA MAMA KAZINI
Na. Dennis Gondwe Dodoma,
WAAJIRI
katika Mkoa wa Dodoma wametakiwa kutoa msukumo katika kurahisisha na kusaidia
wanawake walioajiriwa kuendelea kunyonyesha watoto wao kwa mujibu wa taratibu
ili wawe na lishe bora.
![]() |
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akiongea na mamia ya wananchi |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule katika hotuba yake
kwenye matembezi ya hiari kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama na kusomwa
na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri yaliyoishia uwanja wa Shule ya Msingi
Chang’ombe jijini hapa.
Senyamule
alisema kuwa lengo kuu la maadhimisho ya mwaka huu ni kuongeza uelewa wa jamii
kuhusu umuhimu wa kusaidia wanawake waweze kufanya kazi za uzalishaji pamoja na
utunzaji wa watoto wao. Alisema kuwa ili kufanikiwa “lazima kuhamasisha na
kutetea utekelezaji wa mikakati inayowezesha waajiri kuwa karibu na familia,
walezi au mama wa mtoto na kutoa msukumo katika kurahisisha na kusaidia wanawake
walioajiriwa kuendelea kunyonyesha watoto wao. Kuwahimiza waajiri kutenga
sehemu maalum kwa ajili ya wafanyakazi wanawake wanaonyonyesha ili waendelee
kufanya hivyo mahali pa kazi”.
Alisema
kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuelimisha umma kuhusu sheria ya kulinda haki
za uzazi kwa wanawake na nyingine za kitaifa. “Vilevile, kuwawezesha wanawake
kufanya kazi na kunyonyesha watoto wao ipasavyo kwa kushawishi upatikanaji wa
aina mbalimbali za msaada kutoka kwa wadau katika sekta zote” alisema Senyamule.
Akioanisha
majukumu ya uzalishaji mali, uzazi na maisha ya wanawake na wanaume kwa pamoja,
alisema kuwa kutaleta faida kwenye sekta zote katika jamii. “Faida zinazopatikana
ni pamoja na uboreshaji tija, kipato cha familia na usalama wa kazi, ustawi na
afya ya wanawake na watoto, kufaidika kwa waajiri na kuwepo kwa taifa lenye
mfumo imara wa kijamii na kiuchumi” alisema Senyamule.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa USAID/ Lishe Endelevu unaofadhiliwa na USAID
na kutekelezwa na Shirika la Save the Children, Joyceline Kaganda alisema kuwa mchango
wa mradi katika kufanikisha juhudi za serikali kuhusu afua ya unyonyeshaji wa
maziwa ya mama ikiambatana na ufanyaji kazi kwa ajili ya kujikimu. “Mradi
umewezesha mafunzo na vitendea kazi ili kuimarisha lishe ya wanawake
wajawazito, wanaonyonyesha, watoto wachanga, wadogo na vijana balehe kwa WAJA
wapatao 4,000, Mkoa wa Dodoma peke yake walikuwa WAJA 1,221. Hawa wanatumika
kumfikia mlengwa katika elimu ya unyonyeshaji moja kwa moja hadi ngazi ya kaya.
Mradi pia ulitoa mafunzo ya unasihi wa lishe kwa watoa huduma wa afya 600 na
kwa Mkoa wa Dodoma ni 220 wanaendelea kuimarisha uelewa wa walengwa kila
wanapohudhuria kliniki kuanzia ujauzito na ufuatiliaji wa hali ya lishe ya mtoto”
alisema Kaganda.
![]() |
Mkurugenzi wa Mradi wa USAID/ Lishe Endelevu unaofadhiliwa na USAID na kutekelezwa na Shirika la Save the Children, Joyceline Kaganda |
Fursa
nyingine ya mradi aliitaja kuwa ni kutoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo,
mifugo, na uvuvi kwa maafisa ugani 800 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa
chakula mchanganyiko chenye virutubishi vingi katika ngazi ya kaya na kuongeza
kipato cha kaya. “Sote tutakubaliana ili mama atengeneze maziwa ya kutosha ni
lazima apate mlo wa kutosha na wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi
yote ya vyakula. Pia awe na mahitaji mengine ya msingi ili kumpunguzia msongo
wa mawazo” alisema Kaganda.
Nae
Afisa Lisha wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisema kuwa mama
anayenyonyesha anatakiwa kupunguziwa kazi na msongo wa mawazo. “Siku 1,000 za
mwanzo bora wa mtoto ndiyo maisha bora mtoto, ukikosea hapo mtoto anadumaa kiakili
na uwezo wa kufikiria unadumaa. Hivyo, tunashauri maziwa ya mama mtoto aanze
kunyonya ndani ya saa moja tangu anapozaliwa. Kipindi hiki ndiyo muda maziwa ya
kwanza ya njano yanayokuwa na virutubishi vyote muhimu kwa lishe bora ya mtoto yanauhumu
kwa mtoto. Baada ya hapo endelea kumnyonyesha mtoto kadri anavyohitaji” alisema
Juma.
Maadhimisho
ya wiki ya unyonyeshaji tarehe 1-7 Agosti, 2023 yanaongozwa na kaulimbiu
isemayo “Saidia unyonyeshaji: Wezesha wazazi kulea watoto na kufanya kazi zao
kila siku”.
MWISHO
Comments
Post a Comment