CHEMS YAJIKITA KUZALISHA MADUME BORA YA MBUZI DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
CHEMS
farm imedhamiria kuzalisha madume bora ya Mbuzi aina ya Boha ili kuwasaidia
wafugaji kuboresha mifugo yao ya asili katika kanda ya kati.
![]() |
Mfugaji wa Mbuzi kutoka Chems farm, Vendelin Lyakurwa |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mfugaji wa Mbuzi kutoka Chems farm, Vendelin Lyakurwa
alipokuwa akielezea ufugaji wa Mbuzi katika Banda la Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni
jijini hapa.
Lyakurwa
alisema “lengo la kuzalisha na kuwatunza hawa Mbuzi aina ya Boha ni kuuza
madume kwa wenzetu ili waweze kuboresha mifugo yao ya asili. Ukiwa na dume moja
kwenye boma unaweza kukusaidia kupata mbegu ambayo wanakua haraka na bei yao ni
nzuri na nyama yao ni tamu. Mbuzi hawa ni wa nyama na wanazaa mapacha
ukiwalisha vizuri wanazaa pacha watatu mpaka wanne. Wanakuwa haraka wanasoko
mpaka uarabuni wanawahitaji hawa Mbuzi. Ni Mbuzi ambao ‘wanaadapt’ mazingira
mbalimbali”.
Alisema
kuwa madume wakitumika kwa Mbuzi wa kienyeji wanachukua uzao wa baba. “Wanakuwa
haraka na wanakuwa na nyama nyingi na uzito unakuwa mkubwa ingawa wanakuwa
chotara. Ni Mbuzi wazuri na wanakuwa haraka kwa miezi mitatu kama unamtunza
vizuri anakuwa na uzito wa kilo 22-36 anapoachishwa kunyonya” alisema Mkulima
Lyakurwa.
Alisema
kuwa ameuza mbegu ya madume hao maeneo mbalimbali. “Nimeuza Kigoma, Kagera,
Morogoro, Pwani, Zanzibar, Mtwara na Ruvuma. Ili wakuwe vizuri wanatakiwa kula
vizuri. Ukiwaoteshea majani, uwape na chakula cha ziada kama pumba wanakuwa
haraka na mafanikio yake ni makubwa na kukuletea utajiri wa hali ya juu”
alisema Lyakurwa.
Alisema
kuwa Mbuzi hao wana bei nzuri sokoni. “Nyama yake ni nzuri na inafika shilingi
20,000 sokoni. Akiwa na kilo 100 ukimchinja unapata nyama kilo 55 maana yake
unaweza kumuuza hadi shilingi 1,200,000. Ni wazuri kwa biashara kwa sababu mama
zao wanazaa mapacha kwa miaka miwili wanakuzalia mara tatu” alisema Lyakurwa.
Maonesho ya shughuli za wakulima Nanenane mwaka 2023 yanaongozwa
na kaulimbiu isemayo “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya
chakula”.
MWISHO
Comments
Post a Comment