Ujenzi Queens bega kwa bega na Mwenge wa Uhuru, 2026 Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WIZARA ya Ujenzi inaunga mkono Mwenge wa Uhuru Mwaka
2026 utakaoanza mbio zake tarehe 1 Juni, 2026 katika Wilaya ya Dodoma kwa
kushiriki katika mashindano ya Mwenge Super Cup yakilenga kuhamasisha jamii
kujiandaa na mapokezi ya Mwenge huo kwa kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
Kocha wa Timu ya Wizara ya Ujenzi (Ujenzi Queens), Mwamvita Mzee
Kauli hiyo ilitolewa na Kocha wa Mchezo wa Mpira wa
Pete wa Timu ya Wizara ya Ujenzi (Ujenzi Queens), Mwamvita Mzee alipokuwa
akiongea na mwandishi wetu muda mfupi kabla ya kuanza mchezo wao na Timu ya Mpira
wa Pete ya Dodoma Jiji katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Mzee alisema kuwa hamasa ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026
kwa wanamichezo ni kubwa katika Wilaya ya Dodoma. “Sisi Timu ya Mpira wa Pete
ya Wizara ya Ujenzi tumehamasika kuja kuunga mkono ujio wa Mwenge wa Uhuru
Mwaka 2026 katika Wilaya ya Dodoma. Lengo ni kuonesha umoja na mshikamano baina
ya wanamichezo kama dhamira ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 ilivyo ya kuleta
umoja na mshikamano wa kitaifa” alisema Mzee.
Kwa upande wake Afisa Michezo Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Neema Kilongola alisema kuwa mashindano ya Mwenge Super Cup yanalenga
kuwahamasisha wanamichezo na wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi ya
Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 katika Wilaya ya Dodoma. Hamasa hiyo ni pamoja na
kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote yatakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026.
Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 unaongozwa na kaulimbiu
isemayo “Tanzania ni Yetu Sote,
Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo”.
MWISHO
Comments
Post a Comment