Wasimamizi miradi Jiji la Dodoma watakiwa kuwa wazalendo
Na. Faraja
Mbise, DODOMA
Wasimamizi wa
miradi ya ujenzi katika Shule ya Sekondari Matumbulu wametakiwa kuwa wazalendo
na kutokwamisha juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan, katika kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Kauli hiyo
ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipokuwa akikagua
miradi ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Matumbulu iliyopo katika Halmashauri ya
Jiji la Dodoma.
“Matamanio ya
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuleta hizi shule ni kwasababu watoto
wasitembee umbali mrefu. Bado sisi Mkoa wa Dodoma tuna utoro na baadhi ya
changamoto inayochangia utoro ni watoto kutembea mwendo mrefu kwenda shule.
Kwahiyo, anaona fahari asiende shuleni. Lakini tuna ukatili wa kijinsia, kati
ya maeneo ambayo watoto wanafanyiwa ukatili ni akiwa anaenda shuleni, wanapita
maporini kwasababu ya umbali mrefu, yote haya Rais ametaka ayamalize kwa
kuwajengea shule karibu na eneo lao” alisema Senyamule.
Kwa upande
wake, Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi, alitoa rai kwa wafanyakazi
kuweka mbele uzalendo ili kuhakikisha miradi hiyo inasonga mbele kwa wakati na
kwa viwango vya juu. “Ni rai kwa wenzangu na mimi mwenyewe, tuweke
mbele uzalendo ili tuweze kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati, kwa
viwango vilivyokusudiwa na kuzingatia thamani ya fedha ili tuweze kufikia lengo
lililokuwa limekusudiwa” alitoa rai Mbugi.
Mradi huo wa
ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Matumbulu unatarajiwa kukamilika ifikapo
Desemba 31, Mwaka huu. Shule hiyo ilitengewa jumla ya Shilingi Milioni Mia tano
arobaini na nne, laki mbili, ishirini na tano elfu na mia tano ishirini na sita
(544,225,526) kwa ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na madarasa
nane na ofisi mbili yanayogharimu shilingi 192,628,542, Jengo la Utawala
shilingi 71,491,667, Maabara ya Fizikia 50,000,000 Maabara ya Baiolojia na
Kemia 100,000,000, Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
56,969,143, Choo shilingi 18,700,000, Kichomea taka 3,833,333 na Tanki la maji
3,641,667.
MWISHO
Comments
Post a Comment