Watoto kulindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia wilayani Dodoma
Na. Asteria Frank, DODOMA
Afisa Ustawi wa Jamii wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rachel Balisidya amewataka wazazi kuwalinda
watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanaweza kutimiza
ndoto na malengo yao kwa kuzuia madhara yanayoweza kuwaharibia maisha
kisaikolojia.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma ambae ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rachel Balisidya akihutubia katika Tamasha la (TASHMEKU)
Wito huo aliutoa leo alipomuwakilisha
Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma kwenye Tamasha la Tanzania Shiriki Malezi
Endelevu Kupinga Ukatili (TASHMEKU) katika Shule ya Sekondari Dodoma Makulu
kwa lengo la kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Balisidya alisema kuwa Wilaya
ya Dodoma bila ukatili inawezekana. Alisema kuwa ipo changamoto ya ukatili kwa
watoto na asilimia kubwa ya ukatili inaanzia nyumbani kupitia baba, mama, mjomba,
mwalimu na wale wanaowazunguka na kuwaharibu watoto kisaikolojia kwa kuwatesa,
kubakwa na kuwanyima haki zao za msingi. “Tuhakikishe katika kipindi hiki cha
likizo tuendelee kutoa elimu kwa wazazi ili kulinda usalama wa watoto na
kuwalinda na wale watu wanaofanya ukatili juu yao. Wazazi wanatakiwa kuhakikisha
wanakuwa karibu na watoto wao ili kuwalinda na waweze kuwaambia ukweli kuhusu
jamii ilivyo kwa sasa” alisema Balisidya.
Kaimu Afisa Mtendaji wa
Kata ya Dodoma Makulu, Method Karoly aliwaomba wazazi kupinga ndoa za utotoni
kwa sababu wanawaumiza watoto wanaozaliwa kwa kutopata malezi mazuri kutokana
na wazazi wenyewe kuwa wadogo na wapo chini ya umri wa miaka 18 na kukosa
malezi bora. Alisema kuwa ndoa za utotoni pia ni ukatili wa kijinsia na kuliko
waolewe ni bora watoto wapewe elimu ili iweze kujisaidia wao wenyewe. “Watoto
wanaoingia kwenye ndoa za utotoni wanakutana na mambo mengi sana ya ajabu na
hivyo, akili zao zinaharibika mpaka wanakuwa wanashindwa hata kuwalea watoto
wao na wanachukulia ndoa za utotoni ni za kawaida na kuwafanyia hivyo kizazi
chao pia”. alisema Karoly.
Wanafunzi wa Shahada ya Sheria Mwaka wa Pili Chuo Kikuu cha Dodoma, Jamal Mwasanjala
Nae, Wanafunzi wa Shahada
ya Sheria Mwaka wa Pili Chuo Kikuu cha Dodoma, Jamal Mwasanjala alisema madhara
wanayopata watoto wanaofanyiwa ukatili ni pamoja na kupata tatizo la afya ya
akili, huzuni na kushidwa kuongea mambo ya msingi akiwa na watu. “Asilimia
kubwa watoto wengi wanakuwa na tatizo la afya ya akili kwasababu malezi
waliyopewa ni malezi magumu unaweza kushangaa mtoto anakaa na mzazi wake lakini
anashindwa kuongea hata na mzazi kuhusu tatizo au madhara na chanzo cha
unyanyasaji mtoto aliopitia” alisema Mwasanjala.
MWISHO
Comments
Post a Comment