Naibu Meya Chibago afurahia Kampeni ya Upandaji Miti Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA MAKULU
Naibu Meya wa Halmashauri Jiji la Dodoma,
Fadhili Chibago amefarijika na kampeni ya upandaji miti inayofanywa na
wanariadha wanaotumia baiskeli katika kuzienzi falsafa za Baba wa Taifa, Mwl.
Julius Nyerere ya kupambana na adui wa maendeleo kwa kuondoa ujinga, maradhi na
umasikini.
Naibu Meya wa Halmashauri Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago akielezea kufurahia kampeni ya upandaji miji |
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akimkaribisha
Katibu Tawala wa Mkoa, Kaspar Mmuya katika zoezi la upandaji miti na ugawaji
madawati katika Shule ya Msingi Dodoma Makulu, jijini Dodoma lililofanywa na
wanariadha kutokea Dar es Salaam wakielekea Butiama.
Chibago alisema kuwa amefarijika sana na
kampeni ya wanariadha hao wa kuendesha baiskeli, upandaji miti ikiwa ni falsafa
moja wapo ya kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere katika falsafa
zake tatu za kupambana na maadui wa maendeleo ambao ni ujinga, umaskini na maradhi.
“Jiji la Dodoma tumefarijika sana na kampeni ya hawa ndugu zetu wanayoendelea
nayo pamoja na wadhamini. Wamefanya kitu kizuri sana, nimeona kuna zoezi la
kupanda miti. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Makamu wa Rais, wanatamani Dodoma iendelee kuwa ya kijani” alisema Chibago.
Adha, aliwashukuru wanariadha kwa mchango
wao wa madawati 100 kwa Shule ya Msingi Dodoma Makulu ambayo yatapekea
wanafunzi kukaa na kusoma kwa uhuru zaidi ili kuboresha elimu yao. “Madawati
yatawafanya watoto wetu wakae vizuri na kusoma kwa uhuru zaidi” alisema.
Naibu Meya wa Halmashauri Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago akimwagilia maji mtu alioupanda |
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma
Makulu, Mwl. Amon Sebyiga alitoa shukrani kwa wanariadha na wadhamini kwa
kuweza kutatua changamoto iliyokuwepo shuleni hapo ya upungufu wa madawati hali
ambayo ilipelekea wanafunzi kukaa zaidi ya watano katika dawati moja. “Tunapenda
kutoa shukrani zetu kwa hawa ndugu zetu wa Twende Butiama kwa kutupatia msaada
wa madawati 100 ambayo tutakabidhiwa hivi punde. Idadi hii itaenda kupunguza
mbanano mkubwa wa wanafunzi darasani” alisema Mwl. Sebyiga.
Wakati huohuo, Mwalimu wa Shule ya Msingi
Dodoma Makulu, Denis Thadey alipongeza wanariadha na wadhamini wa madawati
shuleni hapo kwa mchango wao mkubwa kwa kuondoa changamoto iliyokuwapo hapo
shuleni kwa muda mrefu. Changamoto hiyo ilipelekea wanafunzi kubanana katika
dawati moja na hivyo kukosa uhuru wa kusoma nakuandika vizuri. “Nimefurahishwa
na tukio hili la wenzetu ambao wameamua kuendesha baiskeli kutoka Dar es Salaam
kwenda Butiama kwa ajili ya kuenzi kumbukizi ya Mwl. Nyerere. Ujio wao umekuwa
wa mafanikio makubwa sana katika shule yetu. Wametusaidia kuondoa changamoto
tuliyokuwanayo shuleni kwa muda mrefu, wanafunzi walikuwa wanasomea chini,
lakini kwa kushirikiana na wadhamini Vodacom na Stanbic Bank tumeona msaada wao
na moyo wao wa upendo” alisema Mwl. Thadey.
Nae mwanafunzi wa Shule ya Msingi Dodoma
Makulu, Christian Samson aliipongeza serikali kwa misaada ambayo wanaendelea
kutoa shuleni hapo kwasababu inawasaidia katika kukuza taaluma shuleni hapo. “Serikali
haituachi nyuma, tumefurahia sana madawati na tunashukuru kwa umoja wenu”
alisema Samson.
Timu ya waendesha baiskeli |
Zoezi hili la upandaji miti na ugawaji
madawati 100 kwa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, lilihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa serikali pamoja na mashirika binafsi kama Vodacom na Benki ya Stanbic
na wanariadha wa msafara wa baiskeli
uitwao "Twende Butiama" kutokea Dar es Salaam kwenda Butiama kwa
udhamini wa Vodacom na Benki ya Stanbic kwa lengo la kumuenzi Baba wa taifa
katika falsafa yake ya kupambana na maadui wa maendeleo na kugawa madawati
zaidi ya 1,000 kwa shule shule 13,
kupanda miti zaidi ya 50,000, kukabidhi vifaa kwa wanafunzi wenye
mahitaji maalumu na kuendesha kambi za afya kwa mikoa mitano ikiwemo Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment