Twende Butiama kupambana na ujinga, umasikini na maradhi Jiji la Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA MAKULU
Waendesha baiskeli wamuenzi Baba wa Taifa,
Hayati Mwl. Julius Nyerere kwa lengo la kupambana na maadui watatu wa maendeleo
ambao ni maradhi, umasikini na ujinga kwa kugawa madawati 100 katika Shule ya
Msingi Dodoma Makulu iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwenyekiti wa msafara Twende Butiama
Gabriel Landa, alisema kuwa msafara huo una lengo la kumuenzi Baba wa Taifa kwa
vitendo kwasababu Mwl. Julius Nyerere alitumia chombo cha baiskeli wakati alipokuwa
mwalimu na hata alipoacha uwalimu na kuanza harakati za kupigania uhuru na
mambo mbalimbali alitumia baiskeli. Mwalimu Nyerere pia aliwahi kusafiri kwa kuendesha
baiskeli kutoka Dar-es-Salaam hadi Arusha, aliongeza.
Msafara huo umewaunganisha watu wa nchi
mbalimbali kwa kuonesha Mwalimu Nyerere alikuwa sio mbinafsi bali mpenda umoja.
“Wengi wanaotuona barabarani wanahisi haya ni mashindano ila haya sio
mashindano bali ni msafara wa kawaida ambao tunaendesha baiskeli kwa mwendo wa
upendo ambao ni mwendo wa taratibu” alisema Landa.
Aidha, Landa aliongeza kwa kusema, wameamua
kumuenzi kutokana na falsafa yake ya kupinga maadui wa maendeleo kwa
kushirikiana na taasisi binafsi kwa kuzisaidia shule mbalimbali ili kupunguza
changamoto na adha wanazozipata wanafunzi na walimu wakiwa darasani. “Kupitia
wadau mbalimbali tumeweza kukabidhi madawati zaidi 1,000 katika shule zaidi ya 13
hadi kufikia mwaka jana. Lakini tumeweza kupanda miti zaidi ya 50,000 na
kuhamasisha watanzania kujali afya zao kupitia programu mbalimbali” aliongeza.
Msafara huo wa waendesha baiskeli ulitokea
Dar-es-Salaam tarehe 30 Septemba, 2024 na kufika Dodoma Oktoba Mosi 2024 majira
ya jioni. Msafara unajumuisha rika zote kuanzia wazee miaka 60, vijana na
watoto wakitokea maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na Zanzibar nan chi jirani
za Kenya, Burundi, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
MWISHO
Comments
Post a Comment