Twende Butiama wakabidhi Madawati 100 SM Dodoma Makulu
Na. Asteria Frank, DODOMA MAKULU
Watu wasiopungua 90 washiriki kwenye msafara wa Twende
Butiama wakiendesha baiskeli kutoka Dar-es-Salaam na kwenda Butiama kwa lengo
la kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Nyerere waliwasili jijini Dodoma
katika Shule ya Msingi Dodoma Makulu na kugawa madawati 100 na kushiriki zoezi
la kupanda miti.
Msafara huo ulianza safari tarehe 30 Septemba kutoka
Dar-es-Salam na unatarajiwa kufika Butiama tarehe 13 Oktoba, 2024 ukidhaminiwa
na Vodacom pamoja na Benki ya Stanbic walikabidhi madawati 100 na kupanda miti
katika Shule ya Msingi Dodoma Makulu.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya aliupokea msafara
huo wa Twende Butiama na alisema kuwa, upandaji miti unaunga falsafa ya kutunza
Mazingira. Alisema kuwa utoaji wa madawati shuleni unaugana na falsafa ya Mwl.
Julius Nyerere ya kuangamiza maadui watatu wa maendeleo ikiwemo ujinga, umasikini
na maradhi.
Alisema kuwa, kitendo wanachofanya ni kizuri kwa
Tanzania cha kumuenzi Baba Taifa kwa kuendesha Baiskeli kutoka Dar-es-Salaam
mpaka Butiama kinaonesha uzalendo. “Nimeambiwa safari hizi zimefanyika zaidi ya
miaka sita huku mkisema tunamuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo ni ukweli nimeona
wakati ulivyokuwa unatambalisha hapa sio Tanzania tu ni zaidi ya Tanzania na
hayo ndio maisha alikuwa akiishi Mwl. Julias Kambarage Nyerere hakuwa mbinafsi,
alikuwa anapenda umoja” alisema Mmuya.
Aidha, Naibu
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago alisema kuwa Jiji la
Dodoma tumefarijika sana kwa kuwapokea Twende Butiama kwa baiskeli kwakuwa
wamefanya kitu kizuri na kwa zoezi la kupanda miti kwa maana Mheshimiwa Rais,
Dkt. Samia Suluh Hassan na Makamu wa Rais watamani Dodoma iendelee kuwa kijani.
Alisema kuwa upandaji wa miti unaunganisha falsafa ya
viongozi wa nchi. Kitendo cha kupeleka madawati kitawafanya watoto wanaposoma waelewe
vizuri. “Tunawashukuru na tuwakaribishe sana Dodoma kwakuwa Dodoma ni fahari ya
watanzania na ni mahali pa kuishi. Pia Zabibu nzuri inapatika huku karibuni sana”
alisema Chibago.
Nae Mwenyekiti wa Msafara wa Twende Butiama, Gabriel
Landa alisema kuwa wanatarajia kufika Butiama tarehe 13 Oktoba, 2024 kwa lengo
la kumuenzi Hayati Baba wa Taifa kwa vitendo na kwaajili ya kuadhimisha miaka
25 ya kumbukizi ya kifo chake tarehe 14 Oktoba, 2024.
Alisema kuwa Msafara huo umezingatia jinsi zote mbili
ya wanawake na wanaume bila kusahau watoto chini ya miaka 20. Pia umejumuisha
waendesha baiskeli kati yao Tanzania Bara kutoka Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Tabora,
Mbeya, Iringa, Geita, Mwanza, Katavi na Dodoma. Kwa upande wa Tanzania Visiwani
ni Uguja na Pemba. Nchi jirani za Kenya, Burundi, Malawi na Congo zinashiriki,
aliongeza.
“Kuna falsafa nyingi sana alituachia Baba wa Taifa na
moja wapo ya kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni ujinga, umasikini
na maradhi. Tumekuwa tukifanya hayo kwa
kipindi chote tangia tumeanza mwaka 2019
na kupitia wadau mbalimbali tumeweza kukabidhi madawati zaidi ya 1,000 katika
shule zaidi ya 13 hadi kufikia mwaka jana. Lakini pia tumeweza kupanda miti
zaidi ya 50,000 na kuhamasisha watanzania kujali afya” alisema Landa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, Mwl. Amon
Sebyiga alisema kuwa anawashukuru Twende Butiama kwa kutukabidhi madawati 100
kati ya madawati 212 yaliyo kuwa pungufu katika shule yake.
Alisema kuwa madawati hayo yataenda kupunguza
msongomano wa wanafunzi kukaa watano kwenye dawati moja. “Jamii ya Dodoma Makulu
na watu wanaozunguka eneo hili nawatakia safari njema ndugu zetu wa Twende Butiama”
alisema Mwl. Sebyiga.
MWISHO
Comments
Post a Comment