Serikali yaboresha mazingira ya uwekezaji Jiji la DOdoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan imetengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwavutia
wenye viwanda kuwekeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kukuza uchumi.
Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abeid Msangi
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Uwekezaji,
Viwanda na Biashara Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abeid Msangi alipokuwa
akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka mitatu
ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma.
Msangi alisema kuwa kwa mazingira mazuri ya
uwekezaji yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita, Halmashauri ya Jiji la
Dodoma itaendelea kunufaika na uchumi wake kuanza kutegemea viwanda. “Katika
kwenda sambamba na ongezeko la uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, tumejitika
kufuata maelekezo ya Mpango Kabamba wa Jiji la Dodoma. Mpango huo umepanga
maeneo kadhaa ya uwekezaji yakiwepo ya viwanda vikubwa kule Nala. Eneo la
uwekezaji wa viwanda lina zaidi ya ekari 1,500 na viwanja zaidi ya 241. Sehemu
ya viwanja hivyo, imetolewa kwa ajili ya ‘Export Processing Zines Authority’ (EPZA).
Pia wapo wawekezaji wengine wa kati na wakubwa” alisema Msangi.
Alisema kuwa katika eneo la viwanda Nala kimejengwa
kiwanda kikubwa cha mbolea Itracom chenye uwezo wa kuzalisha tani 1,000,000 za
mbolea kwa mwaka. “Kiwanda hicho ni ‘icon’ kwa sasa kinazalisha tani 400,000.
Kiwanda hiki kinaifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mbolea na muuzaji
katika soko la Afrika Mashariki na Kati. Kiwanda hiki kimeweza kubadilisha
kabisa uchumi wa Dodoma. Kitakapokamilika kabisa kinatarajiwa kutoa ajira rasmi
zaidi ya 400 na wale wanaopata fursa kupitia kiwanda hicho kufikia 15,000”
alisema Msangi.
Mafanikio mengine alisema kuwa halmashauri
inajivunia kuanza kujengwa kiwanda kingine kikubwa kitakachokuwa kinazalisha na
kuchuja mbegu za mafuta ya alizeti, ufuta na karanga. ”Kiwanda kinajengwa eneo
la Veyula na kitakuwa na uwezo wa mchujo mara mbili. Kiwanda kitaweza kukamua
alizeti tani 200 kwa siku na kuzalisha mafuta yenye mchujo mara mbili tani 100
kila siku. Kiwanda kikikamilika kitaweza kuajiri wafanyakazi kati ya 500-600”
alisema Msangi.
Msangi
alisema “ndani ya miaka mitatu tumeshuhudia
mabadiliko makubwa, mfano leseni za viwanda vidogo zimebadilika zaidi ya mara
mbili katika kipindi cha miaka mitatu. Tulitoa leseni 242 mwaka 2020 hadi
kufikia mwisho wa mwaka 2023 tumetoa leseni za viwanda vidogo 582. Yote hii
inaonesha mazingira bora yaliyojengwa na serikali ya awamu ya sita yameweza
kuvutia uwekezaji katika hii sekta lakini pia kuongeza nafasi za ajira na
kuongeza pato la taifa”.
Muonekano wa Soko la wazi la Machinga
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya jambo kubwa
katika kutambua mchango wa machinga. Halmashauri imetambua machinga zaidi ya 3,000
na kuwajengea soko kubwa kwa shilingi bilioni 9.5 na mazingira yao ya kufanya
biashara ni mazuri na salama, aliongeza.
MWISHO
Comments
Post a Comment