Jiji la Dodoma lapata hati safi miaka mitatu mfululizo
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inajivunia kupata
hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya
wataalam na Baraza la Madiwani katika kusimamia na kudhibiti matumizi sahihi ya
fedha.
Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu na Fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA. David Rubibira alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu
na Fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA. David Rubibira alipokuwa
akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa miaka mitatu ofisini
kwake.
CPA. Rubibira alisema “kwa bahati nzuri kwa kipindi
cha uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imekuwa ikipata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo. Hati inaangalia maeneo
yafuatayo. Ukaguzi wa hesabu zilizowasilishwa na ukaguzi wa vitabu vilivyofanya
malipo, nyaraka, viambata vyote na mchakato wa ukusanyaji mapato kama
ulizingatia sheria, kanuni na taratibu. Hivyo, hati safi inatokana na
muunganyiko wa hesabu kwamba umefuata viwango vya kimataifa na kuonesha ukweli”
alisema CPA. Rubibira.
Alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano
baina ya wataalam na Baraza la Madiwani. “Wataalam wanawajibu wa kufuata
sheria, kakuni na taratibu za fedha wanapotekeleza majukumu yao na waheshimiwa
madiwani wanawajibu wa kuisimamia halmashauri ili iweze kutekeleza majukumu
yake. Hivyo, ushirikiano huu ndio unapelekea halmashauri kupata hati safi”
alisema CPA. Rubibira.
Mafanikio mengine alitayaja kuwa ni katika eneo la
ukusanyaji mapato ya ndani. “Mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri ilikisia
kukusanya jumla ya shilingi 43,616,465,99, lakini iliweza kukusanya makusanyo
halisi shilingi 44,279,552,980 sawa na asilimai 102. Mwaka wa fedha 2022/2023
halmashauri ilikamisia kukusanya shilingi 55,127,359,997 lakini iliweza
kukusanya makusanyo halisi shilingi 44,639,819,472.12 sawa na asilimia 81. Mwaka
2023/2024 halmashauri ilikamsimia kukusanya shilingi 58,640,360,000 mpaka
kufikia mwezi Machi, tumeshakusanya shilingi 32,760,459,121 sawa na asilimia
54.7. Kwa mikakati ambayo halmashauri imejiwekea kufikia tarehe 30 Juni,
tunatarajia kuwa tumefikisha asilimia 100 ya makusanyo halisi” alisema CPA.
Rubibira kwa uhakika.
Akiongelea mapokezi ya fedha za miradi ya
maendeleo, alisema kuwa shilingi 29,654,533,199 zilipokelewa kutoka serikali
kuu na wadau wa maendeleo. “Fedha hizo zilitekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo
ujenzi wa hospitali ya wilaya, vyumba vya madarasa, ujenzi wa shule, vituo vya
afya, zahanati, nyumba za watumishi na matundu ya vyoo. Fedha hizo zilisaidia
sana katika kuchochea maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akiongelea ukusanyaji wa mapato ya ndani alisema
kuwa yanakusanywa vizuri. “Ndugu waandishi wa habari, ukusanyaji wa mapato ya
ndani unakwenda vizuri. Asilimia 40 inatumika kuendesha halmashauri na asilimia
60 inatumika kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa kipindi cha miaka mitatu
mfululizo tumeweza kutenga jumla ya asilimia 60 ya mapato ya ndani
tuliyokusanya kwenda kwenye miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na asilimia 10
kwenye mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Fedha za
miradi ya maendeleo zimepekwa kwenye uchangiaji wa ujenzi wa barabara, kujenga
vituo vya afya, madarasa na zahanati, ofisi za kata na mitaa. Hivyo, unaweza
kuona kwa kiasi gani mapato ya ndani yamechangia kuleta maendeleo katika
kipindi cha miaka mitatu” alisisitiza CPA. Rubibira.
Mkuu huyo wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu
aliwashukuru wananchi kwa kulipa kodi na tozo za halmashauri kwa hiari na kwa
wakati. Aliahidi kuwa halmashauri itaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya
Habari, matangazo na mikutano mbalimbali ili wananchi wapate elimu ya aina ya
kodi na tozo za halmashauri wanazotakiwa kulipa ili waweze kulipa kwa hiari.
“Hivyo, niwasihi wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari, shughuli zote za
maendeleo mnazoziona katika jamii ni matokeo ya kodi zenu. Wananchi mkiona
wanafunzi wanaenda kwenye shule nzuri, madarasa mazuri, wanakalia madawati,
wakienda hospitali huduma nzuri, dawa zipo mashine za vipimo zipo, ndiyo
matunda ya ulipaji kodi” alisema CPA. Rubibira kwa tabasamu.
Aidha, aliwataka kudai risiti ya mashine ya
kielekroniki (EFD) wanaponunua bidhaa. “Ndugu waandishi wa habari, nisisitize
kwa wananchi wanaponunua bidhaa kuhakikisha wanapewa risiti za kielektroniki
(EFD) na kama wanalipa tozo za halmashauri wahakikishe wanapata risiti ya POS”
alisisitiza CPA. Rubibira.
Kitengo cha Uhasibu na Fedha kina jukumu la
kukusanya maduhuli ya serikali na kusimamia matumizi kwa mujibu wa sheria,
taratibu na kanuni.
MWISHO
Comments
Post a Comment