TANESCO Ddodoma kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme Jiji la Dodoma
Na. Mwandishi Wetu-DODOMA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma limetoa semina kwa
madiwani wa kata zote 41 za Jiji la Dodoma lengo likiwa ni kueleza mikakati ya
shirika hilo pamoja na miradi inayotekelezwa katika Mkoa wa Dodoma.
Akitoa elimu jijini Dodoma, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi
Donasiano Shamba alisema kikao hicho kimejumuisha Madiwani, Kamati ya Usalama
Wilaya na Polisi kata wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Kikao hiki kimehusisha madiwani kutoka kata zote 41 za Jiji la Dodoma
pamoja na Polisi kata lengo ni kueleza mikakati yetu lakini pia kueleza
changamoto zinazotukabili sisi kama shirika hasa suala la uharibifu wa
miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme” alisema Mhandisi Shamba.
Aidha, alisema kwa kuwashirikisha madiwani hao kwenye kikao hicho
watakuwa wamewafikia watu zaidi ya 700,000 wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Dodoma
hakuna uhaba wa umeme bali shida iliyopo ni ubovu wa miundombinu ambayo
inachangia kukatika kwa umeme mara kwa mara, aliongeza.
Alielezea kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 Shirika la
Umeme Tanzania Mkoa wa Dodoma, limetengewa kiasi cha Shilingi bilioni 14, kwa
ajili ya kupeleka nishati hiyo kwa wananchi na kukarabati miundombinu ili
kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme.
“Katika mwaka huu wa fedha tumepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 14 na
kati ya hizo bilioni sita ni kwa ajili ya kuboresha miundombinu yetu na kiasi
kingine ni kwa ajili ya kupeleka umeme maeneo ya karibu na wananchi” alisema Mhandisi
Shamba.
Awali Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Madega Dudu, alisema
shida inayowakabili hivi sasa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya
kusafirishia na kusambazia umeme. "Hivi sasa kumekuwepo na shida ya wizi
wa vyuma kwenye miundombinu ya kusafirishia (Grid) umeme, mafuta ya transfoma,
nyaya za kopa pamoja na miundombinu ya usalama kwenye mashine umba (Transfoma).
Tunaomba wananchi kutoa taarifa dhidi ya watu hawa ambao wanajihusisha na
uharibifu wa miundombinu hii, tafiti zinaonyesha mafuta ya transfoma wanayoiba
kwa kiasi yanachanganywa na mafuta ya kukaangia chipsi lakini pia mikoa ya
kanda ya ziwa na bahari yanatumika kukaangia samaki. Na wengine wanayatumia kwa
ajili ya vipodozi na kiasi kikubwa yanatumika kutengenezea vilainishi vya
mitambo” alisema Dudu.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof.
Davis Mwamfupe alilipongeza shirika hilo Mkoa wa Dodoma kwa kuboresha huduma ya
nishati katika mkoa huo na kuendelea kuwafikia wateja kwa wakati pindi
inapotokea changamoto yoyote.
"Sisi kama Madiwani tunawapongeza TANESCO Mkoa wa Dodoma kwa
kuendelea kutoa huduma bora ya nishati Mkoa wa Dodoma hakuna changamoto kubwa
ya umeme hata inapotokea mnatatua kwa wakati na kuwafikia wateja wenu kwa
wakati kwa hilo tunawapongeza sana" alisema Prof. Mwamfupe.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Charles Mamba
aliyekuwa mgeni rasmi akifunga semina hiyo aliwataka madiwani kwenda kuwa
mabalozi wazuri katika kusimamia miundombimu ya umeme kwa kutoa elimu kwa
wananchi wa maeneo yao.
"Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, DKt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwajali wananchi
wake kwa kuwaletea huduma bora za nishati na kwa mikakati ya TANESCO hapa Makao
Makuu ya nchi, shida ya umeme inaenda kuwa historia" alisema Mamba.
Chanzo Blog ya Michuzi
Comments
Post a Comment