Kata ya Chamwino yatakiwa kuchukua tahadhari ya Kipindupindu

Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefurahishwa na muitikio wa wakazi wa Kata ya Chamwino kushiriki katika mazoezi ya usafi wa mazingira na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu.

Mkuu wa Kitengo cha Usafi na udhibiti taka ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro akiongea na mamia ya wakazi wa Kata ya Chamwino


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na udhibiti taka ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Kata ya Chamwino waliojitokeza kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Kimaro alisema “nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wakazi wa Kata ya Chamwino kwa jinsi mlivyojitokeza kwa wingi kufanya usafi katika eneo la makaburi ya Hijra na maeneo mengine ya kata. Tulichokifanya hapa ni ibada tosha kwa sababu tumesafisha eneo tulipowalaza ndugu zetu. Lakini niwapongeze kwasababu mmekuwa mkijitokeza kwa wingi kufanya usafi katika makazi na maeneo yanayowazunguka”.

Wakazi wa Chamwino wakishiriki zoezi la usafi


Akiongelea tahadhari ya ugonjwa wa kipindupindu aliwataka wakazi hao kuendelea kuchukua tahadhari. “Ndugu zangu, tuendelee kufanya usafi kwenye makazi yetu, amesema hapa mwenyekiti wetu kuwa tunatoa tahadhari kwa ajili ya ugonjwa wa kipindupindu. Na tumaini mmesikia kwenye vyombo vya habari kuwa ugonjwa wa kipindupindu upo katika baadhi ya maeneo nchini. Serikali imeshaanza kutoa tahadhari na halmashauri tunaendelea kusisitiza juu ya tahadhari hiyo. Ndugu zangu uwepo wa kipindupindu unatokana na uchafu na hasa kula kinyesi. Maana yake kuna sehemu usafi haukufanyika vizuri ukaacha nzi wakaingia kwenye vyakula na sisi tukala tukapata kipindupindu. Hivyo, jinsi ya kujikinga ni kufanya usafi kwenye makazi yetu” alisisitiza Kimaro.

Kwa upande wake Mkazi wa Kata ya Chamwino, Mwanaidi Juma alisema kuwa Halmashauri ya Jiji imejitahidi kutoa elimu juu ya usafi wa mazingira. “Niseme ukweli, suala la usafi na umuhimu wake tumeelezwa sana na halmashauri. Ni jukumu letu kufanya usafi wa mazingira. Natamani ifike wakati suala la usafi wa mazingira liwe ni utamaduni wetu na siyo kusubiri serikali kutuhamasisha kufanya usafi. Mfano bwana Kimaro kaongelea suala la kipindupindi, mtu akipata kipindupindu, inayoathirika ya kwanza ni familia yake na mtu akifa hawezi kurudi. Maana yake ni bora kuchukua tahadhari ya usafi ili tuendelee kuwa salama” alisema Juma. 

Usafi wa pamoja siku ya Jumamisi umefanyika katika Kata ya Chamwino ukihusisha maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mamia ya wakazi wa kata hiyo na Mbunge wa Jimbo la Urambo alikuwa sehemu ya washiriki.

Mbunge wa Urambo Mhe Magreth Sitta (kushoto) akifurahia jambo na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na uthibiti wa taka ngumu Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro baada ya kushiriki zoezi la usafi wa mazingira


MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri