Jiji la Dodoma lakemea utapishaji maji taka


Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imekemea tabia ya baadhi ya wakazi kutapisha vyoo kipindi cha mvua na kusababisha kinyesi kwenda kwenye maji yanayotumiwa na wananchi.




Maji taka


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na udhibiti wa taka ngumu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Kata ya Chamwino waliojitokeza kufanya usafi wa pamoja siku ya Jumamosi.

Kimaro alisema “kuna tabia imeibika kwa baadhi ya wakazi wa Kata ya Chamwino kutapisha vyoo. Ndugu zangu tabia hiyo halikubaliki kutapisha vyoo kwa sababu mvua inaponyesha inasomba kile kinyesi na kupeleka kwenye vyanzo vya maji. Maji hayo tunayatumia sisi wenyewe kwa matumizi ya kawaida. Nitumie nafasi hii kuwataka wenye tabia hiyo waache mara moja na tukikukamata tutakuchukulia hatua kwa mujibu wa sheria”.

Mkuu wa Kitengo cha Usafi na udhibiti wa taka ngumu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro akitoa karipio


Alisema kuwa eneo la Kata ya Chamwino kuna mtandao wa maji taka wa Malmaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma mjini (DUWASA). “Naomba pale mtakapoona kuna tatizo la mfumo wa maji taka mtoe taarifa mapema ili wenzetu waweze kulifanyia kazi. Maana tukiacha hivyo, itakuwa chanzo cha ugonjwa wa kipindupindu. Aidha, tunapokula chakula tule cha moto, tunawe mikono kwa maji na sabuni na hiyo ndiyo iwe tabia yetu. Tunafahamu usafi ni ustaarabu na unaanza na mimi” alisema Kimaro.

Wakati huohuo, alivitaka vikundi vya kuzoa taka katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutimiza wajibu wao wa kuzoa taka kwenye makazi kwa wakati. “Nitoe wito kwa vikundi vya uondoshaji taka kwenye makazi ya watu kutimiza wajibu wao. Mimi sitasita kushauri kata kuondoa kikundi ambacho hakifanyi vizuru katika uondoshaji taka. Vikundi vyote tulivyovipa dhamana ya kuondoa taka kwenye makazi ya watu viondoshe taka na visiwe sababu ya kutusababishia ugonjwa wa kipindupindu kwenye makazi ya watu. Hatuwezi kukubali kipindupindu kutokea makao makuu ya nchi” alisisitiza Kimaro.

Kwa upande wake Mkazi wa Kata ya Chamwino, Mwanaidi Juma alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejitahidi kutoa elimu juu ya usafi wa mazingira. “Niseme ukweli, suala la usafi na umuhimu wake tumeelezwa sana halmashauri. Ni jukumu letu kufanya usafi wa mazingira. Natamani ifike wakati suala la usafi wa mazingira liwe ni utamaduni wetu na siyo kusubiri serikali kutuhamasisha kufanya usafi. Mfano bwana Kimaro kaongelea suala la kipindupindi, mtu akipata kipindupindu inayoathirika ya kwanza ni familia yake na mtu akifa hawezi kurudu. Maana yake ni bora kuchukua tahadhari ya usafi ili tuendelee kuwa salama” alisema Juma. 

Usafi wa pamoja siku ya Jumamisi umefanyika katika Kata ya Chamwino ukihusisha maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mamia ya wakazi wa kata hiyo na Mbunge wa Jimbo la Urambo alikuwa sehemu ya washiriki.



MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma