WAZIRI SILAA ASIMAMISHA MATUMIZI YA KITUO CHA MAFUTA CHA BARREL DAR ES SALAAM
Na Eleuteri Mangi, WANMM
Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amesimamisha matumizi ya Kituo
cha Mafuta cha Barrel Petrol Energy cha Mikocheni jijini Dar es salaam na
kupiga marufuku ujenzi holela wa vituo vya mafuta nchi nzima vinavyojengwa
kwenye makazi ya watu hatua inayohatarisha usalama wa watu na mali zao.
Waziri Silaa ametoa
agizo hilo Desemba 23, 2023 alipoenda kukagua eneo kilipojengwa kituo hicho na
aliambatana na Kamati ya ulizi na usalama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
salaam.
"Kufuatia agizo
hili, nawaagiza Wakuu wote wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji nchi nzima wafanye
uhakiki wa vituo vya mafuta kwa maana ya viwanja, mabadiliko ya matumizi ya
ardhi, mchakato uliotumika, ukubwa wa viwanja, ukaribu wa kituo kimoja na vituo
vingine na ukaribu wa maeneo mengine ya kutolea huduma za jamii, hali ya
uendeshaji wa vituo hivyo, taarifa hiyo ifike ofisini Januari 31, 2024"
amesema Waziri Silaa.
Pia Waziri Silaa
amewaagiza wafanyabiashara ya mafuta nchini wafanye uhakiki wa vituo vyao na
Mafuta, mchakato wa namna walivyopata ardhi wanayotumia na kuwasilisha taarifa
hiyo Ofisini kwake ifikapo Januari 31, 2024.
Aidha, Waziri Silaa
amesema ni vema watumishi wa Ardhi na wafanyabiashara hiyo waheshimu Sheria za
nchi kwa vitendo kwa kuwasikiliza watu wasio na sauti ili wapate haki zao
katika masuala ya ardhi.
"Rais Samia
Suluhu Hassan ni mtu wa haki, anataka watu wapate haki, ameniteua mimi
kusimamia haki, hebu tusimamie Sheria, kwa mdomo tukisema tunamuunga mkono
Dkt.Samia Suluhu Hasan, lakini tufanye kwa vitendo kwa kuwasililiza wale 'the
voiceless, sisi tumewekwa hapa kuwa voice of the voiceless" amesema Waziri
Silaa.
Naye mkaazi wa eneo
hilo la Mikocheni Bw. Stephen Rupia amesema wananchi wa eneo hilo
hawakushirikishwa kwenye hatua yeyote ambayo ilitakiwa wananchi washirikishwe.
"Tupo hapa eneo
hili lilikuwa na ukuta na miti mbele na lilikuwa eneo la mtu kwa matumizi yake,
hatukuona bango la kubadilisha matumizi ya eneo hili kujenga kituo hiki cha
mafuta" amesema Bw. Rupia.
Akizungumza kwa niaba
ya mmiliki wa kituo hicho cha Mafuta Mhandisi Stanley Kitundu amesema
wameyapokea maelekezo ya Mhe. Waziri mwenye dhamana ya ardhi na watayatekeleza
na kuongeza kuwa kituo chao kimekamilika kwa asilimia 100 lakini kilikuwa
hakijaanza kufanyakazi.
Comments
Post a Comment