WIZARA YA ARDHI YAZINDUA MFUMO RASMI WA KUWAHUDUMIA WANANCHI “ARDHI APP”
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua mfumo rasmi wa kuwahudumia wananchi popote walipo kupitia simu ya kiganjani “Ardhi App” wa kuwasilisha malalamiko ama migogoro ya ardhi katika wizara hiyo.
Akizindua mfumo
huo Desemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na
Wahariri wa Vyombo vya Habari kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa
amesema, mfumo huo ni rafika na utawarahisishia wananchi kupata huduma wakiwa
katika maeneo yao popote walipo.
“Mfumo huu wa “Ardhi App” utakuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wetu, utapunguza gharama na muda wa wananchi kupata huduma katika maeneo mbalimbali nchini, badala yake mwananchi atapata huduma za ardhi kiganjani mwake” amesema Waziri Silaa.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa, mfumo huo pia utawasaidia wananchi kutoa mrejesho wa ubora wa huduma walizopatiwa pamoja na kuwasilisha tena malalamiko husika pale ambapo hawajaridhika na majibu ama jinsi walivyohudumiwa.
Aidha, ameuelezea mfumo huo kuwa ni rafiki na utasaidia wananchi kuambatisha nyaraka na vielelezo vya malalamiko yao na kuondoa upotevu wa nyaraka pamoja na kupunguza urasimu katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema uzinduzi wa mfumo huo ni moja ya maboresho makubwa yanayofanywa na Wizara ya Ardhi katika kuwahudumia wananchi kwenye sekta ya ardhi.
Uzinduzi huo umeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Geophrey Pinda, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Bi Lucy Kabyemera, wajumbe wa menejimenti wa wizara hiyo pamoja na wahariri wa vyombo vya Habari nchini.
Comments
Post a Comment