RAIS, DKT SAMIA ATOA BIL 4.5 KULIPA FIDIA WANANCHI DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni
4.5 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi 469 wa maeneo mbalimbali katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
![]() |
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, John Kayombo alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya
awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Uzinduzi
wa Mikutano ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na
Waandishi wa Habari katika kampeni ya Tumekusikia Tumekufikia uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Kayombo alisema “Mheshimiwa Rais kwa upendo wake
ameleta fedha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi waliochukuliwa
maeneo yao kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Jumla ya wananchi 469 wanatarajia
kulipwa kuanzia sasa, fedha tumezipokea tayari”.
Akiongelea changamoto ya ‘double allocation’, alisema
kuwa Rais alielekeza wananchi hao wafidiwe viwanja vyao. “Jumla ya viwanja 4,000
vilikuwa vinadaiwa, tumeshatoa viwanja 1,105 kwa wananchi. Bado viwanja 2,895
ametoa fedha za upimaji wa maeneo mapya baada ya upimaji kukamilika wananchi
hao watalipwa viwanja vyao”.
Akiongelea utatuzi wa migogoro ya ardhi, alisema kuwa
halmashauri inatekeleza huduma kupitia kliniki ya ardhi. “Tulianzisha Kliniki
ya Ardhi ambayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanayosimamiwa na Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Wiki iliyopita katika kutekeleza kliniki hiyo
tulifanikiwa kutoa hati miliki 1,474 kwa wiki moja na tulifanikiwa kusikiliza
wananchi 4,005 kwa wiki moja, ni zoezi endelevu tutafanya kila mwezi kwa muda
wa wiki moja.
Wakati akifungua mkutano huo, Waziri wa Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema kuwa program hiyo ni
muhimu kuzungumzia maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. “Serikali ya
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekusikia imekufikia, wale wafanyakazi waliokaa
miaka kadhaa mshahara haujapanda tumekusikia tumekufikia, wale waliokuwa
wanateseka na maji safi na salama hayapo, tumekusikia tumekufikia, wale ambao
ilikuwa ni lazima kumsafirisha mgonjwa wake kumpeleka Dar es Salaam kwenda
kutibiwa tumekusikia tumekufikia, ni kampeni rahisi na inaeleka” alisema Waziri
Nnauye.
MWISHO
Comments
Post a Comment