SERIKALI YATOA BIL 1 UJENZI HOSPITALI YA WILAYA DODOMA
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI imetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya
ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma kwa lengo la kuboresha huduma za afya
na kuzisogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.
Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo akiongea na waandishi wa habari |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, John Kayombo alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya
awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Uzinduzi
wa Mikutano ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na
Waandishi wa Habari katika kampeni ya Tumekusikia Tumekufikia uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Kayombo alisema “kwa upande wa afya mheshimiwa rais
ameleta fedha nyingi. Ameleta shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa
Hospitali ya Wilaya ya Dodoma inayojengwa eneo la Nala. Kituo cha Afya Makole kimekuwa
kikipokea watu wengi sana, mheshimiwa Rais ametuletea shilingi milioni 750 kwa
ajili ya kukipanua na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Vilevile,
ametuletea fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya ya Afya
Chang’ombe”.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema kuwa program hiyo ni muhimu
kuzungumzia maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. “Serikali ya Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan imekusikia imekufikia. Wale kima mama walikuwa na shida ya
kujifungua tumekusikia tumekufikia. Wale ambao ilikuwa ni lazima kumsafirisha
mgonjwa wake kumpeleka Dar es Salaam kwenda kutibiwa tumekusikia tumekufikia,
ni kampeni rahisi na inaeleka” alisema Waziri Nnauye.
MWISHO
Comments
Post a Comment