KAMATI YA SIASA MKOA WA DODOMA YAPONGEZA USIMAMIZI UJENZI SHULE YA MIYUJI B
Na. Dennis Gondwe, MIYUJI
KAMATI ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma imepongeza
usimamizi mzuri wa shule mpya inayojengwa ya Miyuji B iliyopo Kata ya Miyuji
jijini Dodoma na kusema kuwa shule hiyo itawapunguzia hadha ya kutembea umbali
mrefu wanafunzi.
![]() |
Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga akisisitiza jambo |
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi
Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga alipoongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma
kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya Miyuji B inayojengwa
Kata ya Miyuji.
Mbaga alisema “nimpongeze mkuu wa shule jirani ya Miyuji
anayesimamia ujenzi wa shule hii kwa kazi nzuru na usimamizi mzuri. Hakika
majengo ni mazuri na yanapendeza. Aidha, niwapongeze na wahandisi kwa kusimamia
vizuri shule hii. Maeneo mengine wahandisi hawasimamii miradi ya ujenzi jambo
linalopelekea miradi mingi kujengwa chini ya kiwango kwa kukosa usimamizi”.
Vilevile, kiongozi huyo wa Kamati ya Siasa ya Mkoa
wa Dodoma alielezea kufurahishwa kwake kwa taarifa ya shule kutambua mchango wa
nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule hiyo.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa shule mpya
Miyuji B, Mkuu wa Shule ya Sekondari Miyuji, Greyson Maige alisema kuwa shule
hiyo inakwenda kuwaondolea hadha wanafunzi ya kutembea umbali mrefu na kufika
shuleni kwa wakati. Faida za mradi huu utakapokamilika ni kuwasaidia wanafunzi watatembea umbali mfupi na kufika
shule kwa wakati. “Faida nyingine ni kupunguza idadi ya wanafunzi Shule ya Sekondari
Miyuji ilipo Kata ya Mnadani na kupunguza mimba za utotoni pamoja na utoro wa
wanafunzi. Kwa upande wa walimu watakaa kwenye mazingira ya shule na hivyo
kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuwezesha mazingira mazuri ya kuishi
kwa walimu” alisema Mwl. Maige.
Mwl. Greyson Maige akisoma taarifa ya ujenzi wa shule mpya ya Miyuji B |
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo alisema kuwa ulianza kutekelezwa Mwezi Agosti,
2023 baada
ya taratibu zote za manunuzi kukamilika na ujenzi unatekelezwa kupitia mfumo wa
“Force Account”. “Mradi huu unahusisha
miundombinu ifuatayo:- Ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa yenye ofisi mbili, jengo
la utawala, maabara tatu na jengo la maktaba. Mingine ni jengo la Tehama, Vyoo
vya wanafunzi matundu nane na tanki la maji la ardhini. Utekelezaji wa mradi
umefikia asilimia 95 ikiwa kazi mbalimbali za umaliziaji
zinaendelea ambazo ni upakaji rangi,
marumaru na usafi” alisema Mwl. Maige.
Matumizi ya fedha za mradi alisema kuwa Shule ya Sekondari Miyuji
ilipokea kiasi cha fedha shilingi 544,225,626
tarehe 30 Juni, 2023 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya katika Kata ya Miyuji
iliyopo eneo la Mpamaa kupitia mradi wa SEQUIP (Mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu). “Mpaka sasa kiasi
cha shilingi 468,225,626 kimetumika”
alisema Mwl. Maige.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri
alisema kuwa eneo la ujenzi wa shule hiyo limechaguliwa kimkakati katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kwa kuwa katikati ya maeneo ya wananchi na karibu na eneo
zitakapojengwa nyumba 3,500 na Wakala wa Ujenzi Tanzania.
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akielezea umuhimu shule hiyo |
“Niwapongezi Diwani wa Kata ya Miyuji na Mkuu wa
shule ya Miyuji kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hii. Tulishauri pia
kisima kuchimbwa katika eneo kwa lengo la kupata maji ya uhakika. Jukumu la
wazazi sasa ni kuwapeleka shule watoto wao na kutafsi elimu watakayoipata
kwenye fursa ya ajira” alisema Alhaj Shekimweri.
Ikumbukwe kuwa Shule ya Sekondari Miyuji ipo Kata ya Mnadani ambayo
inahudumia wanafunzi kutoka Kata ya Mnadani na Kata ya Miyuji. Idadi ya
wanafunzi katika shule ya Sekondari Miyuji ni 1,467 kati yao wavulana ni 650
na wasichana ni 817 na ina walimu 65.
MWISHO
Comments
Post a Comment