Waziri Mkenda: Michezo na Sanaa shuleni haitaondolewa tena
Na. Denis Mlowe, IRINGA
WAZIRI wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema serikali imejipanga
kuhakikisha michezo na sanaa zinaendelea kupewa nafasi kubwa katika mfumo wa
elimu nchini, akisisitiza kuwa shughuli hizo hazitaondolewa tena shuleni kwa
kuwa ni sehemu muhimu ya kukuza vipaji, afya, ajira na ushindani wa kimataifa.
Waziri Mkenda alitoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Lugalo mkoani Iringa.
Katika hotuba yake,
Waziri Mkenda aliushukuru Mkoa wa Iringa kwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo,
akisema mkoa huo umeendelea kuwa kivutio kutokana na mazingira yake mazuri na
ukarimu wa wananchi wake.
“Tunafurahi sana
kuja Iringa tunawashukuru viongozi na wananchi wote wa Iringa kwa kutupokea na
kuwa wenyeji wa mashindano haya muhimu kwa maendeleo ya michezo nchini,”
alisema.
Aidha, aliwapongeza
wanafunzi, walimu na viongozi wa michezo waliofanikiwa kufika katika hatua ya
taifa baada ya kushinda katika ngazi mbalimbali kuanzia shule, kata, wilaya na
mikoa.
Waziri Mkenda
alitoa pongezi kwa sekretarieti ya mashindano pamoja na wizara na taasisi
zilizoshiriki katika maandalizi ya UMISSETA, akitaja Ofisi ya Waziri
Mkuu-TAMISEMI, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akizungumzia nafasi
ya michezo katika maendeleo ya taifa, Mkenda alisema michezo ni zaidi ya
burudani kwani ni chanzo cha afya bora, mshikamano wa jamii, ajira na fursa za
biashara.
Alisema shule zinapaswa kuendelea kuwa viwanda vya kuzalisha na kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo na sanaa, huku akisisitiza kuwa sera ya elimu inatambua rasmi umuhimu wa kubaini na kuendeleza vipaji mbalimbali mapema.
“Kupitia sera ya
elimu, serikali imeweka wazi kuwa itaendelea kubaini na kuendeleza wanafunzi
wenye vipaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo michezo, sanaa, sayansi na
teknolojia,” alisema.
Mkenda alieleza
kuwa michezo na sanaa za maonyesho zimeingizwa rasmi katika mafunzo ya amali,
sambamba na sekta nyingine kama kilimo, uvuvi na ufundi, hatua inayolenga
kuwajengea wanafunzi ujuzi na uwezo wa kujitegemea.
Akihamasisha
wanafunzi kushiriki kwa bidii katika mashindano hayo, Waziri Mkenda alisema
kaulimbiu ya UMISSETA 2026 inayosema “Michezo na Sanaa, Shule ni Daraja la
Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa” inapaswa kuwapa hamasa ya kuangalia
mbali zaidi ya mashindano ya ndani.
Alisema Tanzania
ina kila sababu ya kuamini kuwa siku zijazo inaweza kufuzu na kushiriki Kombe
la Dunia kupitia uwekezaji unaoendelea kufanyika katika michezo ya shule na
maendeleo ya vipaji vya vijana.
“Ninaamini baadhi
ya watakaocheza Kombe la Dunia katika miaka ijayo wanaweza kuwa miongoni mwa
wanafunzi waliopo hapa leo. Hivyo mshiriki mashindano haya kwa bidii, nidhamu
na kujituma,” alisema.
Aliwataka washiriki
wote kuzingatia usalama, maadili na uadilifu wakati wote wa mashindano,
akisisitiza kuwa mafanikio ya michezo yanategemea nidhamu na kuheshimu sheria
na taratibu.
Kwa upande
mwingine, aliipongeza hatua ya kuwapa wanafunzi nafasi ya kusimamia michezo
kama waamuzi, akisema jambo hilo linasaidia kujenga kizazi cha wataalamu wa
michezo wenye weledi na uwezo wa kusimamia mashindano kwa haki.
Mashindano ya
UMISSETA 2026 yamewakutanisha wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa
lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo na sanaa vinavyoweza kuiwakilisha
Tanzania katika mashindano ya kikanda na kimataifa.
Comments
Post a Comment