Makala: Tanzania inavyojiandaa kuvuna matunda ya AFCON 2027

Na. John Walter, Manyara

Mwezi Juni mwaka 2027 utaingia kwenye historia ya Tanzania kwa maandishi yasiyofutika kirahisi.



Kwa mara ya kwanza tangu kupata uhuru, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano makubwa zaidi ya soka barani Afrika, Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yatakayoandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda.

Kwa wengi, AFCON ni mashindano ya mpira wa miguu yanayodumu kwa siku 30 pekee.

Lakini kwa wachumi, wawekezaji na wafanyabiashara wadogo, ni injini kubwa ya uchumi inayoweza kuingiza mabilioni ya fedha, kuzalisha ajira na kuitangaza Tanzania mbele ya mamilioni ya watu duniani.

Tayari maandalizi yameanza kuonekana kupitia miradi mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkoa wa Arusha, ambao umetajwa kuwa miongoni mwa wenyeji wa mashindano hayo, unashuhudia ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olmot.

Uwanja huo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 30,000 umefikia zaidi ya asilimia 83 ya ujenzi na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2026.

Uwekezaji huo wa miundombinu tayari umeanza kuvutia pongezi kutoka kwa wadau wa soka duniani.

Mwezi Mei 2026, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza na klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand, alipotembelea Uwanja wa Samia Suluhu Hassan unaojengwa Arusha, aliusifu kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya kimataifa.



“Nimecheza kwenye viwanja vingi duniani lakini kiwanja hiki ni kizuri na chenye viwango. Niwapongeze wajenzi, wakandarasi na wataalamu wote wanaofanya kazi hii nzuri,” alinukuliwa akisema wakati wa ziara yake nchini.

Hata hivyo, nyuma ya zege, nondo na vifaa vya kisasa vinavyojenga uwanja huo, kuna ndoto na matumaini ya maelfu ya wananchi wanaotarajia kunufaika na AFCON.

Mubaraka Sungi, mkazi wa Arusha, anaamini mashindano hayo yatafungua milango ya fursa kwa wananchi wa kawaida.

“Wenye hoteli watanufaika, mama ntilie watanufaika, boda boda watanufaika, hata wauza bidhaa za asili watanufaika. Kutakuwa na fedha nyingi zinazozunguka kwa muda mfupi,” anasema. 

Kwa mtazamo wake, AFCON si tukio la michezo pekee bali ni uchumi unaotembea kutoka kwa mgeni mmoja kwenda kwa mamia ya wananchi wanaotoa huduma mbalimbali.

Mtazamo huo unaungwa mkono na Alex Mlai ambaye anaona manufaa ya mashindano hayo yatafika hata katika mikoa inayozunguka Arusha.

“Babati nayo itanufaika. Wageni wengine watatafuta malazi nje ya Arusha, wengine watanunua huduma mbalimbali njiani. Huu ni uchumi wa watu wa kawaida,” anasema.

Katika pembezoni mwa barabara kuu ya Arusha–Babati, Jenipha Alphonce amekuwa akitengeneza na kuuza bidhaa za asili ikiwemo vikapu, mikeka, shuka za Kimasai, kofia na mapambo mbalimbali yanayovutia watalii.

Anasema ukuaji wa sekta ya utalii umeongeza wateja kutoka mataifa mbalimbali tofauti na zamani walipokuwa wakitegemea zaidi wateja wa ndani.

“Sasa tunapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi. Kuelekea AFCON 2027 tunajipanga kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuboresha ubunifu ili wageni watakaokuja wapate huduma bora,” anasema.

Jenipha anaamini bidhaa za asili za Tanzania zitakuwa mabalozi wa kuitangaza nchi kimataifa kwa sababu zinawakilisha utamaduni na urithi wa Watanzania huku zikiwa rafiki kwa mazingira.

Kwa mujibu wa makadirio ya Serikali, Tanzania inatarajia kupokea wastani wa mashabiki na watalii takribani 300,000 kwa siku katika kipindi cha mashindano hayo.

Iwapo maandalizi yatafanyika kwa ufanisi, idadi hiyo inaweza kuongeza kwa kiwango kikubwa matumizi katika sekta za hoteli, usafirishaji, chakula, biashara za fedha, utalii, burudani na mawasiliano.

Uzoefu wa mataifa mengine unaonyesha namna mashindano ya AFCON yanavyoweza kubadilisha uchumi wa nchi mwenyeji.

Morocco, ambayo iliandaa michuano mikubwa ya Afrika kwa mafanikio makubwa, ilivunja rekodi ya watazamaji kwa kuvutia mashabiki zaidi ya 729,000 katika hatua ya makundi pekee. Nchi hiyo ilikadiriwa kupokea kati ya mashabiki 600,000 hadi milioni moja kutoka mataifa mbalimbali na kuingiza zaidi ya Euro bilioni moja kupitia shughuli zilizohusiana na mashindano hayo.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na siasa, Hamduni Marcel, anaeleza kuwa mafanikio ya kiuchumi ya AFCON yatategemea uwezo wa Tanzania kutumia vizuri fursa zinazokuja pamoja na mashindano hayo.

Anasema sekta ya utalii, hoteli, usafiri, biashara za kubadilisha fedha na huduma nyingine zitakuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa.

“Jambo hili halina mashaka kuhusu uchumi kukua. Arusha ni jiji la wachacharikaji. Kinachohitajika sasa ni maandalizi ya pamoja ya taasisi zote husika ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajua fursa zilizopo na wanajiandaa kuzitumia,” anasema.

Anashauri Bodi ya Utalii Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana kwa karibu katika kuitangaza AFCON mapema ili kuvutia wageni wengi zaidi.

Mbali na mapato ya moja kwa moja, AFCON inaacha urithi wa muda mrefu kupitia miundombinu.

Barabara zinazojengwa leo zitatumika hata baada ya mashindano kuisha. Viwanja vya ndege vitabaki kuhudumia wasafiri.

Hoteli zitabaki kupokea wageni. Viwanja vya michezo vitatumika kuibua vipaji vya vijana wa Tanzania kwa miaka mingi ijayo.

Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Zanzibar kupitia Uwanja wa Fumba na Arusha kupitia Uwanja wa Samia Suluhu Hassan vitakuwa vituo muhimu vya mashindano hayo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali imejipanga kuifanya Arusha kuwa kitovu cha michezo nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu na programu za kuendeleza vipaji vya vijana.

Hii inaonyesha kuwa AFCON si tukio la mwezi mmoja pekee, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza michezo, utalii na uchumi wa taifa.

Aidha, Arusha ikiwa lango la utalii nchini, wageni watakaokuja kushuhudia AFCON watapata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya Serengeti, Tarangire,Arusha national Park, Eneo la Hifadhi la Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro.

Hivyo, mashindano hayo yatakuwa maonesho makubwa ya vivutio vya Tanzania mbele ya dunia.

Kwa wafanyabiashara wadogo, huu ni wakati wa kuuza bidhaa, huduma na utamaduni wa Tanzania.

Kwa vijana wanaotafuta ajira, ni fursa ya kupata kipato kupitia sekta mbalimbali zitakazohitaji nguvu kazi ya muda na ya kudumu.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika Mashariki, nchi tatu zimeungana kuandaa mashindano makubwa kiasi hiki. Ushirikiano huo unaimarisha diplomasia ya uchumi, biashara na mahusiano ya kikanda.

AFCON 2027 si mashindano ya soka pekee. Ni mtihani wa uwezo wa Tanzania kutumia michezo kama chachu ya maendeleo. Wakati mashabiki watakapokuwa wakishangilia magoli viwanjani, maelfu ya Watanzania watakuwa wakivuna matunda ya ajira, biashara na utalii.

Na filimbi ya mwisho itakapopulizwa Julai 2027, ushindi mkubwa zaidi huenda usiwe wa nchi itakayochukua kombe, bali w

a Tanzania itakayokuwa imejijengea uchumi, hadhi na fursa mpya mbele ya dunia.  

 

Comments

Popular Posts

Ujenzi wa madarasa 3 S/M Mazengo kukamilika Julai, 2026

Bodaboda Mtaa wa Kigamboni wanufaika na Kliniki ya kutatua kero