DG TANESCO atembelea Banda la EWURA CCC, apongeza utendaji kazi
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Mkurugenzi Mtendaji
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amelipongeza Baraza
la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), kwa mchango
wake katika kupokea, kusaidia na kufuatilia utatuzi wa malalamiko ya watumiaji
wa huduma za nishati na maji, hatua inayosaidia huduma zinazodhibitiwa na EWURA
ikiwemo huduma ya umeme kuboreshwa kwa maslahi ya wananchi.
Twange ametoa pongezi hizo leo, Juni 19, 2026, baada ya kutembelea banda la EWURA CCC katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akizungumza katika
banda hilo, Twange amesema kazi inayofanywa na EWURA CCC ya kupokea,
kusaidia na kufuatilia utatuzi wa malalamiko ya huduma za umeme imekuwa chachu
ya maboresho ya huduma hiyo, ikiwemo kupungua kwa baadhi ya changamoto
zilizokuwa zikilalamikiwa mara kwa mara.
“Tunatambua mchango
mkubwa wa EWURA CCC katika kuwawakikisha wananchi na kufuatilia utatuzi wa
changamoto zao. Malalamiko mnayotupatia yanatusaidia kutambua maeneo
yanayohitaji maboresho na kuchukua hatua stahiki ili kuendelea kuwahudumia
wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Twange.
Kwa upande wake,
Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa EWURA CCC, Amani Mbogo, amesema idadi
ya malalamiko yanayohusu TANESCO imeendelea kupungua ikilinganishwa na miaka
iliyopita, ambapo sehemu kubwa ya malalamiko hayo yalihusiana na huduma za
kuunganishiwa umeme.
EWURA CCC inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kutetea watumiaji wa huduma za nishati na maji kwa kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wa mtumiaji, kupokea malalamiko ya watumiaji na kuwaelekeza utaratibu wa utatuzi wake.
Aidha, EWURA CCC
imekuwa ikifuatilia malalamiko hayo ili kuhakikisha yanatatuliwa kwa wakati na
mamlaka husika kwa ustawi wa watumiaji na kufanya huduma ziwe bora na endelevu.
Chanzo: Fullshangwe Blog
Comments
Post a Comment