Ujenzi wa miundombinu ya Barabara yarahisisha usafiri kwa wananchi Mtumba
Na. Leah Mabalwe, MTUMBA
Kata ya Mtumba yanufaika na ujenzi wa barabara pamoja
na kalavati kwa gharama ya shilingi 73,000,000 kwa lengo la
kurahisisha upatikanaji wa usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje
Hayo
yalielezwa na Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo kuona miradi ya maendeleo mbalimbali
iliyotekelezwa na serikali kwa kipindi cha miaka minne.
Diwani
Maboje alisema kuwa kata yake imepata miundombinu mizuri ambayo inasaidia
usafiri kupatikana kwa urahisi. “Katika kata hii ya Mtumba tulikuwa na
changamoto ya ubovu wa barabara kwa kiasi kikubwa, hususan barabara za Mtaa wa Vikonje
pamoja na barabara kutoka Mtumba Kibaoni hadi Shule ya Msingi Mtumba na hali
hii ilikuwa ikiwapa changamoto wakazi wa mtaa huo kwasababu hapo mwanzo mvua
zilipokuwa zikinyesha watu walikuwa wakipata shida kuvuka na kwenda sehemu
nyingine” alisema Maboje.
Aliongeza
kuwa wananchi wa Kata ya Mtumba wanafuraha kubwa kupata miundombinu hiyo. “Serikali
imetuletea jumla ya shilingi 73,000,000 kwaajili ya ujenzi wa barabara hizi.
Niseme kwamba toka ujenzi huu wa kalavati pamoja na kutengeneza barabara uanze
ingawa sio kwa kiwango cha lami imeweza kuwarahisishia wananchi kuvuka na
kwenda sehemu nyingine kwaajili ya kufuata mahitaji na hata wasafirishaji
wanaweza kusafirisha watu pamoja na bidhaa kiurahisi” aliongeza Maboje.
Kwa
upande wake mwananchi Cosmas Kanjongo alisema kuwa anaishukuru serikali kwa
kuwajengea barabara ambayo inawasaidia kusafiri kwa haraka. “Kutokana na ujenzi
huu wa kalavati pamoja na barabara hapa kwetu, tumesaidika sana. Kwanza kabisa
hili kalavati linatusaidia kwa msimu huu wa mvua hatukupata madhara makubwa
kwasababu linaruhusu maji kupita kiurahisi kuelekea sehemu zingine. Na hii
barabara ilivyoboreshwa inatusaidia kwasababu inapitika kiurahisi, tunaweza
kupitisha mizigo yetu kuelekea barabara kubwa” alisema Kanjongo.
Naye
Celina Chibada aliipongeza serikali kwa kutatua changamoto ya barabara ambayo
imeleta msaada kwa wanawake na watoto wanaotumia barabara hiyo. “Kabla ya ujenzi huu wa barabara kulikuwa
hapapitiki na mvua zilivyokuwa zinanyesha pikipiki zilikuwa hazipiti, sisi
wanawake na watoto tulikua tunateseka sana kupita. Kwa sasa tunaishukuru sana
serikali kwa kutujengea hii barabara pamoja na kalavati tunanufaika nayo sana”
alipongeza Chibada.
MWISHO
Comments
Post a Comment