Vijana waalikwa kushiriki Kongamano S/M Mbwanga

Na. Mwandishi Wetu

Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujitokeza na kushiriki kongamano la vijana la Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 lenye lengo la kutoa elimu kuhusiana na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kongamano la Vijana katika mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025, Abeid Msangi

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kongamano la Vijana katika mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025, Abeid Msangi akiongelea maandalizi ya kongamano hilo litakalofanyika katika Shule ya Msingi Mbwanga iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alisema kuwa kongamano hilo limeandaliwa kwa ajili ya vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Nichukue nafasi hii kuwahamasisha vijana wa Jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kongamano hilo. Kongamano hilo linalenga kuwajenga vijana kuwa wazalendo, kuifahamu historian a falsafa ya Mwenge wa Uhuru. Pia tutatoa elimu kwa vijana kuhusiana na umuhimu wa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa amani na utulivu. Mada nyingine zitakazofundishwa ni fursa za kiuchumi katika sekta ya madini pamoja na fursa zilizopo Halmashauri ya Jiji Dodoma. Vilevile, vijana watahamasishwa katika masuala ya afya ili waweze kulitumikia taifa wakiwa na afya njema” alisema Msangi.

Akiongelea vijana wanaolengwa katika kongamano hilo, aliwataka kuwa ni vijana mchanganyiko kutoka katika vyuo, sekta binafsi na wajasiriamali na kusisitiza kuwa hakuna ubaguzi. “Nipende kuwataarifu vijana kukimbilia fursa za namna hii kwasababu zinajitokeza kwa mara moja kila mwaka tunapokuwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru. Fursa hizi ni muhimu kwasababu kuna vitu vingi vya kujifunza kama vijana, lakini pia mafunzo hayo yatawapatia faida kutokana na kitu mlichojifunza” alisema Msangi.

Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 ulianza rasmi mbio zake katika Mkoa wa Dodoma tarehe 20 Aprili, 2025 na katika Wilaya ya Dodoma utapokelewa na kukimbizwa tarehe 26 Aprili, 2025 chini ya kaulimbiu isemayo “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri