Afisa Elimu Sekondari Jiji la Dodoma atoa wito wananchi kujitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru, 2025
Na. Leah Mabalwe, VIWANDANI
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Mwl. Zainabu Abdallah amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki
mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 na kuushangilia katika maeneo yote
utakapopita hasa katika Shule ya Sekondari Miyuji B utakapoweka jiwe la msingi
shule hiyo.
Aliyasema hayo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2025.
“Nipende kuwahamasisha wananchi wote wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 na kuukimbiza
katika maeneo yote Jiji letu la Dodoma. Tunawategemea sana wananchi kwasababu Mwenge
wa Uhuru ni mali yetu sote, tujitokeze na tushirikiane kuukimbiza katika maeneo
yote” alisema Mwl. Abdallah.
Alisema kuwa miongoni mwa miradi itakayotembelewa
ni Shule ya Sekondari Miyuji B. Mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi ujenzi
wa mabweni mawili, vyumba vinne vya madarasa na matundu 10 ya vyoo, aliongeza.
Mwl. Abdallah ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Mapokezi na Malazi alisema kuwa kamati yake imejipanga vizuri. “Katika
maandalizi ya kupokea wageni ambao watashiriki katika kuukimbiza Mwenge wa Uhuru,
tumejiandaa vizuri katika kuwapokea wageni wetu muhimu ili wapate sehemu nzuri
ya kupumzika na kwaajili kupata afya nzuri ili kuukimbiza Mwenge wa Uhuru wakiwa
na afya njema. Hivyo, tumejiandaa na kujipanga kikamilifu kwa ajili ya mapokezi
haya” alisema Mwl. Abdallah.
Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma utapokelewa tarehe
26 Aprili, 2025 ukitokea Wilaya ya Bahi ukiongozwa na kaulimbiu inayosema
“Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.
MWISHO
Comments
Post a Comment