Serikali yatoa fedha kujenga Kituo cha Jemolojia ili kuongea thamani ya Madini
Na. Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa katika
kuhakikisha Madini yanaongezewa thamani kabla ya kupelekwa nje ya nchi,
Serikali imetoa fedha nyingi na kujenga Kituo kikubwa cha Jemolojia ili kuwa na
kituo bora, chenye mashine bora na wataalam bora nchi nzima ili kuhakikisha
Madini hasa ya vito yanaongezewa thamani hapa nchini kwa viwango
vinavyohitajika kabla ya kusafirisha kwenda nje.
Mhandisi Samamba aliyasema hayo jijini Dodoma katika hafla fupi ya utiaji saini wa makubaliano kati ya Kampuni Sun Set kutoka Tailand na Taasisi ya Jemolojia Tanzania iliyoko chini ya Wizara ya Madini.
Alisema kuwa watahakikisha kwamba wanaweka utaratibu wa namna ambavyo makubaliano hayo yatatekelezwa ili pande zote mbili waweze kunufaika na makubaliano hayo.
“Kupitia Kituo chetu chetu cha TGC, Mheshimiwa Rais ameweka fedha nyingi, tumejenga jengo kubwa kabisa ambacho ni kituo kikubwa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla ambapo lengo ni kuhakikisha tunakuwa na kituo bora, chenye mashine bora, chenye wanafunzi bora na wataalam bora ili waweze kutapakaa nchi nzima kuhakikisha kwamba Madini hasa ya vito yanayotokea nchini yanaongezewa thamani hapa nchini mpaka viwango vinavyohitajika ndio yaweze kusafirishwa nje".
Aidha, alisema kuwa lengo kubwa la kusaini mkataba wa makubaliano haya ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inataka Madini yote yanayochimbwa ndani ya nchi ya aina yote yanaongezewa tahamani ndani ya nchi kabla ya kwenda nje ya nchi.
Naye Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania, Mhandisi Ally Noganga alieleza kuwa dhumuni la serikali kuingia makubaliano na Kampuni ya Sun Set ni kuboresha taaluma ya masuala ya Jemolojia kwa maana ya Sayansi ya Madini ya vito pia kuongeza ubunifu katika suala zima la ukataji na ung'arishaji wa madini ya vito.
Kampuni ya Sun Set inajishughulisha na kununua na kukata madini ya vito lakini kwa wingi madini ya Safaya na Rubi.
Comments
Post a Comment