Mikopo ya asilimia 10 yawang’arisha wajasiriamali Makutupora
Na. Nancy Kivuyo, MAKUTUPORA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kupitia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 yanufaisha makundi ya
wanawake katika kujikwamua kiuchumi katika Kata ya Makutupora ikitajwa kuwa chachu
ya kuinua maendeleo katika sekta ya kilimo, ufugaji na ujasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na makundi ya wanawake waliopata mikopo ya asilimia 10 katika Kata ya Makutupora, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Makutupora, Andrew Boma alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kusimamia vema uwezeshaji wa wananchi kupata haki zao hasa kwa makundi maalum ambayo yamewezeshwa kupitia mikopo hiyo. “Sisi Kata ya Makutupora vikundi 20 vimepatiwa mkopo wa jumla ya shilingi 230,000,000. Vikundi vya wanawake ni 10, vijana saba na watu wenye ulemavu vitatu. Mpaka sasa wameweza kurejesha shilingi 159, 980,000 na bakaa inaendelea kulipwa na vikundi hivyo” alisema Boma.
Aliongeza
kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na shughuli mbalimbali kama useremala,
ushonaji, ufundi ‘welding’ na biashara ya bodaboda ambazo zinawawezesha
kuongeza kipato na kumudu gharama za maisha. “Kimsingi tunamshukuru sana rais
wetu kwasababu ameweza kugusa maisha ya watu wenye uhitaji. Mikopo hii
imesaidia wananchi kuongeza kipato, kununua mahitaji ya watoto, kununua mali
kama viwanja, kumudu gharama za matibabu na kuendesha maisha yao. Kiujumla
serikali, mheshimiwa mbunge na diwani nao wana mchango mkubwa sana kwasababu wamekuwa
wakitusemea huko kwenye vikao na kufanya umoja wao kuwa na mabadiliko chanya
kwa jamii ya Makutupora” aliongeza Boma.
Alisema
kuwa anawajibu wa kuhakikisha shughuli za maendeleo katika kata hiyo zinakuwa
na mafanikio kupitia elimu na uhamasishaji. “Kiukweli maendeleo ya jamii ni
muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla. Mimi hapa Kata ya
Makutupora hakuna eneo naweza kulikwepa, kwasababu mambo yote ya msingi
yanayomgusa na kumjenga mwananchi nayahudumia kwa kushirikiana na watalaam
wengine” alieleza Boma.
Nae, Afisa Mtendaji wa Kata ya Makutupora, Hamisi Jigwa alisema kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa mkombozi kwa wananchi wa Makutupora. “Tunaipongeza sana serikali kupitia rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyajali makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kupitia mikopo hiyo, wanavikundi wamepata faida ambayo inawasaidia kulipa ada za watoto, kununua mahitaji na wengine wamefikia hatua ya kuanzisha miradi mingine iliyotokana na faida. Kwahiyo, niwaase watu wenye uhitaji wa mikopo watembelee ofisi za kata watapata maelekezo namna mikopo hiyo inavyopatikana” alisema Jigwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment