Jiji la Dodoma kutekeleza mradi wa urejeshaji taka
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya JUZA, Nasibu Kitabu kwa kushirikiana na Kampuni ya
Global Waste Solutions watambulisha mradi wa uchakataji na urejeshaji wa taka kwa
Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kupunguza
kiwango cha taka zinazopelekwa katika Dampo la Chidaya.
Aliyazungumza hayo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri na kusema kuwa taasisi hiyo imejikita katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira pamoja na kutoa elimu kwa vijana wanaofanya kazi ya kuzoa taka. “Kwasasa tupo katika Jiji la Dodoma na tumeungana na Global Waste Solutions kufanya hii kazi ili kupunguza kiasi kikubwa cha taka kwenda dampo ifikapo mwaka 2027. Yote hii ni kuweza kuifundisha jamii namna ya kutenganisha taka ili tuweze kuiokoa jamii yetu na changamoto zitokanazo na utunzaji na utupaji holela wa taka” alisema Kitabu.
Aliongeza
kuwa Jiji la Dodoma limekuwa kwa kasi na ndipo ilipo sura ya nchi. “Jili la
Dodoma ni fahari ya watanzania, tumeona ni vema tukaanzia hapa ili kuweka mji
safi lakini pia mazingira ya wananchi yawe salama. Elimu nzuri itasaidia jamii
kujua namna ya kutenga taka kwasababu zipo taka nyingine zinatumika kutengeneza
mbolea na vitu vingine” aliongeza Kitabu.
Alisema
kuwa mradi huo utajikita katika maeneo ya kuhamasisha jamii kutenganisha taka
katika ngazi ya kaya na taasisi na kuhakikisha taka zinazoweza kutumika tena
ziweze kurejeshwa kiwandani. Pia utajikita katika kutenganisha taka ngumu kama
plasitiki na taka oza kama vile mabaki ya vyakula.
Nae, Mtaalam na Msimamizi wa Udhibiti Taka ngumu Global Waste Solutions, Amir Amir alisema kuwa mradi huo wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira umejikita katika maeneo matatu ya Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma na Moshi. “Mradi huu kwa Jiji la Dodoma ni muhimu kwasababu hapa ndio makao makuu ya nchi na tutaanzisha vituo vya kudhibiti taka ngumu ikiwemo plastiki na karatasi na tutaanzisha kituo cha uchakataji wa mabaki ya taka oza ikiwemo vyakula na matunda yanayoharibika katika masoko na majumbani. Kwahiyo, tutatengeneza mbolea ya asili na wadudu watakaotumika kama protini mbadala kwaajili ya vyakula vya mifugo” alisema Amir.
Katika
hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka ngumu Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alieleza kuwa, wamepokea utambulisho wa mradi
wa Taasisi ya JUZA kwa ushirikiano na Global Waste Solutions wa uchakataji na
urejeshaji wa taka. “Sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, eneo hili ni moja ya
maeneo ya kimkakati ambao tulijiwekea kuwa tutashirikiana na wadau mbalimbali
kuhakikisha tunarejesha taka, tunatenganisha taka na kutoa elimu kwa wananchi
wafahamu namna ya kutenganisha taka” alifafanua Kimaro.
Alimalizia
kwa kutoa ahadi ya kushirikiana na wadau hao katika kuhakikisha wananchi wa
Dodoma wananufaika na uwepo wa mradi huo
wa kuliweka jiji safi na salama. “Kipekee kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma, nichukue nafasi hii kuwakaribisha sana nyie wadau wetu, tunawaahidi kutoa
ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba huu mradi katika kipindi cha
miaka miwili unatekelezwa na unakuwa na manufaa kwa wananchi wa Dodoma na
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kiuchumi” alimalizia Kimaro.
MWISHO
Comments
Post a Comment