Senyamule apigilia Msumari matumizi ya Nishati safi ya kupikia
Na. Mussa Richard, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa
wananchi jijini Dodoma kutumia nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na
kulinda afya za wananchi kutokana na madhara ya matumizi ya nishati chafu ya
kupikia.
Senyamule alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara katika Kata
ya Nzuguni, baada ya kufanya ziara na kukagua miradi mbalimbali ya maendelea
katika kata hiyo.
“Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ameshaelekeza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia nyumbani na katika sehemu za mikusanyiko, kwahiyo kama huwezi kununua mtungi wa gesi ni bora zaidi ukatumia nishati mbadala kama makaa ya mawe na kuni poa, kwasababu upatikanaji wake na gharama zake ni nafuu na rafiki kwa kila mmoja wetu kuweza kuzimudu, hilo litasaidia kuondokana na madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya nishati chafu za kupikia, lakini pia itasaidia kutunza mazingira ya jiji letu na kuondokana na uhalibifu kama ukataji wa mkaa” alisema Senyamule.
Nae Jabir Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma akazitaka
taasisi zote kwa pamoja kutumia ipasavyo nishati safi ya kupikia ili kuondoa
madhara ya uharibifu wa mazingira katika Jiji la Dodoma na kuwa mfano kwa
taasisi za mikoa mingine kuiga na hatimaye kuwa na Tanzania inayotunza
mazingira kwa vitendo.
“Katika masuala ambayo serikali ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan imevipa kipaumbele ni sekta ya nishati
safi ya kupikia, kwasababu serikali imeona uharibifu na madhara makubwa ambayo
yanasababishwa na matumizi ya nishati chafu ya kupikia, na mwisho wa kampeni
hii ya kuhakikisha wananchi kote nchini wanatumia nishati safi ya kupikia
ilikua mwisho mwezi Desemba mwaka jana, na nikatoa tamko kuwa hatutarajii tena
kukuta sehemu yenye mkusanyiko wa watu zaidi ya 100 bado wanatumia nishati
chafu ya kupikia kama, mkaa na kuni” alisema Shekimweri.
Comments
Post a Comment