Watumishi Zahanati Kitelela mambo shwari
Na.
Mussa Richard, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Rosemary Senyamule ametembelea na kukagua nyumba ya watumishi wa
Zahanati ya Kitelela iliyopo Kata ya Nzuguni, Wilaya ya Dodoma na kuwataka
watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi.
Nyumba hiyo ‘two in
one’ imegharimu kiasi cha shilingi 60,000,000 hadi kukamilika kwake, ikiwa na
uwezo wa kukaliwa na familia mbili kwa pamoja.
Baada ya kukagua
nyumba hiyo alisema “utekelezaji wa mradi huu ni muendelezo wa utekelezaji wa
maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhakikisha tunapunguza
vifo vya mama na mtoto, hasa wakati wa kujifungua, dhamira ya mradi huu ni
kuimarisha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Mwanzoni huduma za
afya zilikuwa zikitolewa lakini ikifika jioni huduma zinakuwa hazitolewi
kutokana na wauguzi kuishi mbali na kituo cha afya. Lakini kwasasa muda wowote
wananchi wa Kitelela na maeneo jirani wana uwezo wa kupata huduma muda wowote
baada ya mradi huu wa nyumba za wauguzi kukamilika”.
Nae, Alhaji Jabir
Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma akatoa pongezi kwa wananchi wa Kitelela
kwa kukamilika kwa mradi huo, ambao utakuwa mkombozi wa huduma ya afya kijijini
hapo.
“Nitoe pongezi kwa wananchi wa Kitelela kwa kukamilika kwa mradi huu wa nyumba ya mtumishi, kwasababu ni mradi ambao mliuanzisha nyie wenyewe baada ya kuona kuna uhitaji. Kwahiyo, imani yangu ni kuwa mtaendelea kutumia huduma za afya za zahanati hii, moja ya changamoto ambazo bado zipo ni kukosekana kwa huduma ya maji, changamoto ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi kwa kuchimbwa kisima cha maji. Kisima ambacho kitasaidi kupatikana kwa maji ya kutosha katika zahanati” alisema Shekimweri.
“Mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kitelela umesaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi hasa mama wajawazito ambao walikua wanatembea umbali mrefu kufuata huduma na sasa tumewasogezea huduma ya kliniki ya mama na mtoto na wananchi watapata huduma za afya muda wote” alisema Dkt. Sebastian Pima Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kitelela ulianzishwa mwaka 2005, kituo kinapatikana Kata ya Nzuguni Mtaa wa Kitelela, ambapo hapo awali ilikua na majengo mawili ambayo ni jengo la OPD na jengo la ‘Maternity’ ambalo kabla ya mradi kukamilika lilikuwa likitumika kama nyumba ya mtumishi.
MWISHO
Comments
Post a Comment