SHIKUHA yatakiwa kutoa elimu ya haki za Abiria
Na. Asteria Frank, DODOMA
Shirika la Kutetea Haki za Abiria (SHIKUHA)
latakiwa kuwapa elimu ya kutosha abiria kwa lengo la kutatua changamoto za
usalama barabarani na kufanya abiria wajuwe haki na wajibu wao.
Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya
wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa
Rafiki Hoteli Dodoma alipomuwakilisha Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa elimu
itolewe wakati safari inapoanza ili abiria akipata sehemu ya kujitetea wanakuwa
na amani na dereva akienda tofauti na sheria za barabarani waweze kutoa taarifa
kuhusu tukio hilo kwa watu sahihi. “Rai yangu kubwa kama kuna kitu ambacho
ningewahasa nyie kama shirika kulifanya hili basi ni kuwa na mpango mkakati na
huo mpango utaonesha dira yenu kama mlivyosema kwenye risala na lakini mnataka
kufikia wapi mwaka huu na je, tunapimaje viongozi maana nyie ni viongozi wa
kitaifa kwa kutunza na kusaidia abiria” alisema Prof. Mwamfupe.
Mwenyekiti wa Taifa SHIKUHA, Solomon
Nkiggi, alisema kuwa katika kipindi kifupi cha uwepo wa SHIKUHA imefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa abiria kuhusu haki na wajibu wao kwa kuwaelimisha
abiria kupitia semina, mikutano na matangazo ya vyombo vya habari kwa baadhi ya
mikoa. “Changamoto ni nyingi zinazowakabili abiria wetu ikiwemo kupanda kwa
nauli isivyo rasmi, ukosefu wa huduma bora kwa baadhi ya maeneo pamoja na
ukiukwaji wa haki za msingi za abiria. SHIKUHA imejipambanua kama daraja kati
la abiria na watoa huduma za usafiri na serikali kwa lengo la kushughulikia
changamoto hizi” alisema Nkiggi.
Kwa upande wake, Muhasisi wa Utetezi wa
Abiria Tanzania, Hassan Mchangama, alisema kuwa SHEKUHA inatetea abiria wa nchi
kavu na baharini na wamesimamia maeneo yote. Pia watawaelimisha abiria kujua
haki zao mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo za Latra, Usalama
barabarani na kimataifa ikiwemo haki ya kupata fidia mtu anapopata ajali.
“Kwenye eneo la ajali kumekuwa na
changamoto kubwa sana maana abiria wengi hawajui namna ya kufuatilia haki zao au
baadhi ya sheria zimekuwa na changamoto. Matokeo yake abiria wengi nchini
Tanzania wanafariki katika ajali, hawalipwi fidia na wanapata majeraha na
hawapatiwi matibabu na wengine wanapoteza mali. Tunajua haki mbalimbali
zimeimarishwa kutokana na sheria ikiwemo haki ya kusafiri salama” alisema
Mchanjama.
MWISHO
Comments
Post a Comment