DC Shekimweri ahimiza mpango wa lishe bora shuleni
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri aliwataka wakuu wa shule na walimu wakuu kutekeleza mpango wa huduma
ya chakula kwa wanafunzi wote shuleni ili kuhakikisha wanapata lishe bora jambo
litakalopelekea kujifunza kwa ufanisi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri
Aliyasema hayo ofisini kwake wakati
akihamasisha wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuandikisha watoto shuleni
katika ngazi ya awali na msingi pia wale wanaojiunga na kidato cha kwanza kwa
mwaka wa masomo 2025.
Akisisitiza kuhusu mpango wa huduma ya
chakula kwa wanafunzi shuleni, “……kuna uhusiano mkubwa sana kati ya ufaulu na
lishe, mtoto ambaye hajashiba ni ngumu sana kumsikiliza mwalimu akamuelewa na
akazingatia, ni tofauti na mtoto aliyepata chakula shuleni” alisema Alhaj
Shekimweri.
Kwa upande wa wazazi na walezi katika Jiji la
Dodoma walisema kuwa wamepokea vizuri mpango wa huduma ya chakula kwa wanafunzi
shuleni ili kuhakikisha wanapata lishe bora ikiwa ni chachu ya maendeleo ya
wanafunzi kiujumla.
Charles Maganya, mzazi kutoka Kata ya Ihumwa alisema
kuwa mpango huo kama utatekelezwa vizuri utasaidia katika maendeleo ya watoto
wawapo shuleni kwa sababu ili mtoto ajifunze ni lazima awe ameshiba na kuwa
imara kimwili na kiakili. “Ni mpango mzuri na umepokelewa vizuri. Mpango huu
kwa namna moja utakuwa ni chachu kubwa ya maendeleo ya watoto wetu shuleni kwa
sababu watapata nafasi ya kusoma bila shida wakiwa wameshiba” alisema Maganya.
Akiongelea kuhusu kuhakikisha wanafunzi
wanapata lishe bora shuleni, mkazi wa Kata ya Ipagala, Bathseba Njigo,
alifafanua kuwa wao kama wazazi wanahakikisha wanaunga mkono jitihada hizo kwa
kuchangia vyakula shuleni ili kuhakikisha watoto wanakaa darasani wakiwa
wameshiba tayari kwa kupokea kile wanachofundishwa na walimu. “Uzuri ni kwamba
shule nyingi zina utaratibu wa kuchangia chakula, sisi kama wazazi kwa nafasi
yetu sehemu kubwa tunajitahidi kuunga mkono hizo jitihada ili watoto waweze
kukaa darasani wakiwa wameshiba, waweze kupokea kile walimu wanachowapatia” alisema
Njigo.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya wazazi hupuuzia
jambo hilo wakidhania kuwa ni michango isiyokuwa na ulazima. Alisema kuwa
wazazi hao hawawatendei haki watoto wao na wadau wengine wa elimu wanaoweka
jitihada katika kuboresha elimu, ufaulu wa wanafunzi na taifa kwa ujumla.
Nae, mkazi wa Kata ya Ihumwa, Esther Yohana,
aliwashauri wazazi na walezi kujitoa ipasavyo katika kuchangia vyakula na michango
mingine kwa wanafunzi ili kuimarisha mpango wa lishe bora shuleni kwa sababu ni
faida kwa wanafunzi, wazazi na taifa kwa ujumla. “Wazazi tuchangie kwa sababu
ni faida watoto wetu na kwa taifa letu” alisema Yohana.
Wazazi, walimu na wadau wote wa elimu nchini
wanatakiwa kushirikiana ipasavyo katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mahitaji
muhimu shuleni ikiwemo elimu bora na lishe bora ili kuimarisha afya zao kimwili
na kiakili kwa lengo la kutengeneza nguvu kazi ya taifa imara.
MWISHO
Comments
Post a Comment