Wataalam watumike kukuza mapato ya ndani
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Mamlaka
za Serikali za Mitaa zimetakiwa kuwajengea uwezo wa kimbinu na kuwatumia wataalam
wa ndani ili kuongeza mapato ya ndani sambamba na kubuni miradi ya kimkakati
yenye tija kwa maendeleo ya nchi.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko akifafanua jambo kwa mfano
Hayo
yalisemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa
akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, waliotembelea
Dodoma kwa lengo la kujifunza na kuongeza wigo wa namna sahihi ya kuongeza
mapato ya ndani kupitia miradi mbalimbali, katika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Hakuna mapato madogo na hakuna mradi mdogo, ila
tunapoandaa miradi, tujiulize tunaandaa miradi yenye mfumo gani?. Kwahiyo,
tunavyofikiri miradi, hata yenye mtazamo wa kibiashara lazima tufikirie kwenye
kukua kwake. Hivyo, kila kitu kinaweza kikaanza kwenye udogo, kikakua na mapato
yaleyale madogo tunaweza tukaanzisha miradi kwa mapato ya ndani. Nilichokuwa
nataka kusema cha kwanza ni kutumia wataalam ili kutuongoza katika namna bora
ya kutekeleza miradi hiyo” alisema Dkt. Sagamiko.
Akizungumza
kuhusu ziara ya Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, aliwataka
watumie fursa hiyo ya ziara ili kuongeza nguvu katika kutekeleza miradi. “Naomba
ziara hii itumike kuwajenga, kuwaongezea nguvu zaidi, kwamba tulipo tunaweza
kufanya pakubwa zaidi badala ya kuwakatisha tamaa, ni kweli tumekuja kujifunza
miradi. Lakini kikubwa tumekuja kutanua fikra zetu, tupate matamanio ya mambo
ya kwenda kufanya Kyerwa, kikubwa tumekuja kupanua wigo” alisisitiza Dkt.
Sagamiko kwa kauli ya kutia moyo.
Aidha,
aliwataka watumishi wa serikali kukubaliana na maeneo ambayo wamepangiwa kazi,
hata kama yana miundombinu mibovu wasihame na kuwataka wao ndio wawe chachu ya
maendeleo ya sehemu hiyo na kutokimbilia mijini. “Watumishi tuna ‘tendency’
ya kwenda mahali ambapo ni pazuri, lakini hatujui kwamba kuna watu walifanya
kazi mahali pale kuwa pazuri. Dodoma ilikuwa kama Kyerwa, lakini kuna watu wakafanya
kazi, hakuna sehemu yoyote kabla ya uhuru tukasema ilikuwa kama vile ilivyo,
hata Kyerwa hayo maendeleo mnayoanza kuyaona, kasi imeongezeka baada ya kuwa wilaya.
Sisi binadamu wengi tunakuwa wavivu wa kufikiri, wengi tunatamani kwenda
kutumia vya wenzetu kuliko kutengeneza vile tunavyotamani sisi. Tunaona
tunakuja kupata changamoto, watumishi hawashiriki kufanya ‘transformation’
ya maendeleo ili waweze kuyaweka matamanio ya sehemu wanayoishi” alisema Dkt.
Sagamiko.
Sambamba
na hayo, aliwaasa kusimamia miradi ambayo wanaianzisha ili iwe na matokeo
chanya, kutumia mapato ya ndani kwa busara na kufanya uwekezaji popote pale
nchini pasi na kuwa na mipaka.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, kutoka
Mkoa wa Kagera, SACF.
James John, aliipongeza Hamashauri ya Jiji la Dodoma kwa uthubutu wa kufanya
mambo makubwa zaidi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Sanjari
na hayo, alieleza sababu ya kuelekeza ziara yao katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. “Tumetembelea miradi kadha wa kadha,
ambayo imejengwa katika namna tatu. Kwanza, mapato ya ndani, pili, fedha kutoka
serikali kuu na tatu, kutoka ufadhili wa Benki Kuu ya Dunia. Kimsingi miradi
yote imenivutia kwasababu inaonesha tija na hadhi, kilichonivutia zaidi ni
mradi wa Shule ya Dodoma English Medium School, kwasababu inatumia mtaala wa lugha
ya kingereza kufundishia. Kwanini, tumekuja Dodoma, ni kwasababu ya kuwaonesha madiwani
uthubutu waliokuwa nao wenzetu katika Jiji la Dodoma. Jiji la Dodoma sio kuwa
linapata mapato makubwa zaidi nchini Tanzania, lakini wamefanya mambo makubwa
zaidi kuliko halmashauri nyingi, tulichokiona zaidi ni uamuzi na uthubutu wa
wataalam na madiwani katika kutekeleza miradi ya maendeleo” alisema SACF. John.
Akiongelea mambo ambayo amejifunza katika ziara
hiyo, Diwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Devota Biashara, alisema
“katika miradi yote tuliyozunguka, nimevutiwa haswa na mradi wa shule, katika
Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kyerwa nasi tunampango wa kujenga shule itakayotumia
mtaala wa kingereza kufundishia. Kwahiyo, nilipoona mradi huu unaendelea vizuri
na tulipoolezwa, hakika nilifurahi na nilijifunza vitu vingi. Jambo lingine,
nimejifunza uthubutu, tukitaka kuamua kitu tunakuwa waoga, lakini ziara hii
imetujengea ujasiri”
MWISHO
Comments
Post a Comment