Madiwani wadaiwa uthubutu kufanya maamuzi ya kimaendeleo
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa,
mkoani Kagera, wametakiwa kuwa na uthubutu katika kufanya maamuzi ya kimaendeleo
ili kuwanufaisha wananchi wanaowasimamia. Hayo yalisemwa na Mstahiki Meya wa
Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, alipokuwa akiwakaribisha madiwani kutoka
Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
Mstahiki Meya, Prof. Davis Mwamfupe akifafanua jambo
“Kikubwa katika mtakachokiona, sio utajiri
wetu wa pesa ni uthubutu wa kufanya maamuzi, unaweza kuwa na pesa lakini hauna
uthubutu wa kuzitumia, ukipewa shilingi milioni moja, utapata wasiwasi
kuzitumia kwasababu zitaisha, hutakubali matumizi ya laki mbili au tatu. Lakini
sisi hatuogopi, kama tuna mradi wa hoteli iliyopo hapa ambayo imegharimu
shilingi Bilioni 12, hatuogopi mradi wa Soko la wazi la Machinga, ingawa
serikali ilituchangia shilingi Bilioni tatu, na sisi tukaweka shilingi bilioni
sita nyingine. Hatuogopi kwamba tuliwekeza katika mradi na hoteli na ukumbi
kule Mtumba, ambao kwa awamu mbili tulipanga uwe na shilingi bilioni 54. Karibuni
Dodoma muweze kuangalia matokeo ya uthubutu wetu wa kufanya maamuzi. Sisi
hatupendi kujadiliwa kwanini hatukuamua tunapenda tushtakiwe kwanini mliamua
vibaya” alisema Prof. Mwamfupe.
Akizungumzia suala la maendeleo, aliwataka
waheshimiwa madiwani kuunga mkono juhudi za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
katika kukuza uchumi wa nchi na kutoa rai kuwa, wananchi wahudumiwe vizuri bila
kutengeneza kero. “Tuungane na Mheshimiwa Rais, kuhakikisha kwamba, tunafikisha
maendeleo bila kero yoyote kwa wananchi wanaotegemea huduma yetu” alisisitiza
Prof. Mwamfupe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri
ya Wilaya ya Kyerwa, SACF. James John, aliwataka madiwani hao kujifunza namna
mbalimbali za kukusanya mapato kupitia ziara hiyo waliyoifanya ili kukuza uchumi
wa Kyerwa. “Kwanini nilitamani tuje Dodoma, ni kwamba, kuamua ni bora sana
kuliko kusitasita, lakini kuamua kwa manufaa ya taasisi, kwamba leo sisi
tunafanya haya maamuzi makubwa watu hawatatuelewa, watatulaumu lakini kokote
tutakakokuwa miaka ya mbeleni tutasema wakati sisi tuko kwenye halmashauri
tulifanya moja na mbili. Kwahiyo, jambo ambalo natamani tuondoke nalo hapa ni
kuthubutu kufanya bila kujali ‘size’ ya kipato chetu” alisema SACF. John.
Vilevile, Diwani wa Kata ya Matunguru, Halmashauri
ya Wilaya ya Kyerwa, Florence Frederick, aliipongeza Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, kwa kuonesha uthubutu katika kuanzisha na kuendeleza miradi. “Nimejifunza
mambo mengi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kupitia ziara hii, mfano Shule
ya Dodoma English Medium School. Kwahiyo, tumejifunza na sisi tutaenda kufanya
juhudi zetu tuwe na shule nzuri kama hiyo. Naipongeza Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, kwa mipango yake mizuri na mapato wanayopata, inaonekana walithubutu na
sisi tutathubutu ili mambo yaende vizuri” alipongeza Frederick.
Madiwani hao waliwasili Halmashauri ya
Jiji la Dodoma tarehe 17 Desemba, 2024 kwa ajili ya ziara ya siku moja, yenye
lengo la kutembelea miradi ya kimkakati iliyopo jijini Dodoma na kujifunza uthubutu
wa kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo ili kuongeza mapato ya halmashauri
yao.
MWISHO
Comments
Post a Comment