Wananchi wa Dodoma watakiwa kutumia nishati safi kupikia
Na. Valeria Adam, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule
aeleza faida za nishati safi kwa matumizi ya kupikia na kuwataka wananchi wa
Dodoma kuacha kutumia nishati chafu kwa matumizi ya nyumbani na sehemu za kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aeleza faida za nishati safi
Aliyasema hayo katika halfa ya ugawaji wa
mitungi ya gesi na majiko 1,000 kwa shule, zahanati, vituo vya afya, vituo vya makao
ya watoto na mama na baba lishe huku akieleza kuwa hatua hiyo inalenga
kuimarisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia, kuboresha afya za
watumiaji na kulinda mazingira.
Alisema kuwa nishati safi ina faida kubwa kwa
watumiaji na mazingira hatua hiyo inalenga kuimarisha matumizi ya nishati safi
kwa ajili ya kupikia, kuboresha afya za watumiaji, na kulinda mazingira. “Faida
za nishati safi ni pamoja na matumizi bila kuathiri afya za watumiaji. Pia,
itapelekea hewa ya oksijeni kuongezeka na miti kuendelea kukua, na hivyo,
Dodoma itaendelea kuwa salama” alisema Senyamule.
Aliongeza kuwa biashara ya nishati safi ina
fursa kubwa kwa sasa kwasababu watumiaji watazidi kuongezeka, na watu
wataendelea kununua gesi mara baada ya mitungi yao kuisha. “Nishati safi ni
biashara kubwa kwa sababu watumiaji watazidi kuongezeka, lakini pia
watakapomaliza gesi wataendelea kuijaza mitungi, na hivyo matumizi ya gesi
hayataisha” alisisitiza Senyamule.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri alisema kuwa anatamani kuona halmashauri inajumuisha kifungu maalum
kwenye bajeti yake ambacho kitaruhusu taasisi hizo kununua gesi kila mwezi. “Matarajio
yangu kwenye bajeti ya halmashauri itaongeza kifungu mtakachotenga fedha kila
mwezi kwa shule na vituo vya afya viwe na uwezeshaji wa kununua gesi na kujaza
kwenye mitungi” alisema kwa msisitizo Alhaj Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri aliielekeza halmashauri kuweka kifungu kwenye bajeti
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma
Mjini, Anthony Mavunde, alisema kuwa matumizi ya nishati safi yanachangia kwa
kiasi kikubwa kupunguza ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira. “Kwa miaka
ya hivi karibuni, ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira umepungua sana na
kaulimbiu yetu ya 'Kukijanisha Dodoma' imeanza kuzaa matunda. Sasa, ukijani
tumeanza kuuona katika maeneo yetu” alisema Mavunde.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde akielezea umuhimu wa nishati mbadala
Pia, aliahidi kuendelea kuhamasisha matumizi
ya teknolojia za nishati mbadala, pamoja na aina ya mkaa usio na madhara kwa
mazingira, kama ule wa kutumia makaratasi, plastiki, na magome ya miti. “Sisi
kama viongozi ni lazima tuwatoe wananchi wetu kwenye kukata miti kutengenezea
kuni na mkaa na kuwahamasisha kuacha kutumia mkaa na badala yake kutumia
nishati safi” aliongeza Mavunde.
Hatua ya kugawa mitungi ya gesi na majiko
inaonesha dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuhakikisha wananchi wanatumia
nishati safi kwa faida ya afya zao na mazingira huku ikikuza uchumi wa taifa.
MWISHO
Comments
Post a Comment