Jiji la Dodoma latoa Kilo 790 za sukari kwa shule 150
Na. Faraja Mbise, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetoa kilo 790
za sukari kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na sekondari ili kuwawezesha
kupata uhakika wa chai wanapokuwa shuleni ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais
wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini za kuhakikisha nishati safi ya
kupikia inatumika katika taasisi mbalimbali.
Kilo hizo zilitolewa na Naibu Meya wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi
na majiko 1,000 kwa shule, zahanati, vituo vya afya, vituo vya watoto yatima na
mama na baba lishe tukio lililofanyika katika uwanja wa Nyerere square jijini
Dodoma.
Naibu Meya Chibago alisema kuwa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imechangia kilo 790 za sukari kwa shule za msingi na
sekondari 150. Shule za msingi zilizopewa sukari hiyo ni 104 na shule za
sekondari ni 46 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania na mbunge wa
jimbo la Dodoma mjini, aliongeza.
Akiongelea zoezi la utoaji wa majiko na
mitungi 1,000 ya gesi kwa taasisi mbalimbali, alisema kuwa ni jambo la
kizalendo. “Kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kwa moyo
wa unyenyekevu sana tunataka kukushukuru sana kwa moyo wako, bila kusukumwa na
yeyote kwa nia yako ya dhati ya kulipenda Jimbo lako la Dodoma mjini.... Sisi
Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumepokea kwa mikono miwili maoni ya Mheshimiwa Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutamani watanzania wote tuondokane na matumizi ya
kuni lakini pia tutumie sasa nishati mbadala” alisema Chibago.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Dodoma Mlimani, Mwl. Jenifa Mhavile aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma
kwa ugawaji wa sukari na mitungi ya gesi katika shule. Alisema kuwa itawasaidia
kuokoa muda wakati wa kupika chai
ofisini na pia watatoa elimu kuhusu utumiaji wa nishati safi na kuhamasisha utumiaji wa nishati safi ya
kupikia katika vikao vya wanafunzi na wazazi. “Kutokana na kuwa tupo katika
kampeni ya kupinga matumizi ya nishati chafu tutatumia elimu hii kuhamasisha
juu ya matumizi sahihi ya gesi. Tutahakikisha kuwa kila mmoja anakuwa balozi
katika masuala ya matumizi ya gesi” alisema Mwl. Mhavile.
Hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko
1,000 kwa shule, zahanati, vituo vya afya, vutuo vya makao ya watoto na mama na
baba lishe ni kuunga mkono jitihada za Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Halfa hiyo ni ya tatu kwa
Mbunge Anthony Mavunde, ambapo awamu ya kwanza nay a pili alitoa jumla ya
majiko 1,500 kwa lengo la kupunguza matumizi ya nishati chafu ya kupikia ambayo
ina athari kubwa katika mazingira na kupelekea vifo vya watu wengi nchini.
MWISHO
Comments
Post a Comment