Msimamizi wa Uchaguzi Jiji la Dodoma atoa maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa
kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa tarehe 27 Novemba,
2024 ili kuchagua viongozi bora.
Ushauri huo ulitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akitoa Maelekezo ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 kwa waandishi wa habari ofisini kwake leo tarehe 26 Septemba, 2024.
Dkt. Sagamiko alisema “niwahamasishe wananchi wa
halmashauri ya jiji la Dodoma kujitoleza kwa wingi siku ya uchaguzi ambayo ni
jumatano ya tarehe 27 Novemba, 2024 ili kuchagua viongozi bora watakaoongoza”.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema kuwa wananchi wenye
sifa za kushiriki wanatakiwa kushiriki. “Ninatoa wito kwa wananchi wote wenye
sifa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa uchaguzi, kuanzia hatua ya
kujiandikisha kwenye orodha ya mpiga kura. Kujiandikisha katika orodha ya wapiga
kura ni hatua inayompa kila mwananchi mwenye sifa haki ya kisheria kushiriki
uchaguzi kama mpiga kura au mgombea nafasi ya uongozi” alisema Dkt. Sagamiko.
Akiongelea nafasi zitakazogombewa alizitaja kuwa ni
mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa kamati ya mtaa mchanganyiko na kundi la
wanawake. “hivyo, wananchi wenye sifa wanahimizwa kuchukua na kurudisha fomu za
kugombea nafasi hizo kwa tarehe zilizoainishwa katika maelekezo haya. Ushiriki wa
wananchi wengi katika kugombea nafasi hizi ni muhimu katika kukuza demokrasia
na kuhakikisha upatikanaji wa viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu”
alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma
alitoa maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 mbele ya waandishi wa habari,
viongozi wa vyama vya siasa na makundi maalum pamoja na wadau wengine.
MWISHO
Comments
Post a Comment