Maekelezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 yatolewa Jiji la Dodoma
Na. Asteris Frank, DODOMA
Msimamizi wa
Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko ametoa maelekezo
ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 kwa umma.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko akitoa Maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 kwa umma
Akizungumza mbele
ya vyombo vya habari ofisini kwake leo tarehe 26 Septemba, 2024 kuhusu
maekelezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 alisema kuwa Msimamizi wa
Uchaguzi amepewa mamlaka ya kutoa maelekezo kuhusu uchaguzi. “Maelekezo haya
yanatolewa siku 62 kabla ya siku ya uchaguzi, kwa lengo la kuhakikisha kuwa
taratibu zote zinafuatwa na kwamba wapiga kura Pamoja na wagombea wanapata
taarifa zote zinazohitajika kwa wakati. Maelekezo haya yanafafanua hatua
zitakazo ongoza mchakato wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, uchukuaji
na urejeshaji wa fomu za kugombea, uteuzi wa wagombea na tarehe ya siku ya uchaguzi.
Maelekezo haya yanalenga kutoa muongozo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa
uwazi, haki na usawa na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa” alisema Dkt.
Sagamiko.
Aliongeza kuwa
kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi lililotolewa kwa kuzingatia kanuni ya nne ya kanuni
ya uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mtaa (tangazo namba 574),
uchaguzi utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024. Kwa mujibu wa kanuni ya 11 (GN.
Na. 574 (Mamlaka za Miji), zoezi la uandikishaji wa wapiga kura litafanyika
kuanzia tarehe 11-20 Oktoba, 2024 katika vituo vilivyopangwa, aliongeza.
Akiongelea sifa
za kupiga kura kwa wakazi alisema kuwa umri kuanzia miaka 18. “Kwa mujibu wa
kanuni ya 13 GN. Na. 574 wakazi wote wenye umri wa miaka 18 au zaidi na
waliokidhi masharti ya kisheria wanahimizwa kushiriki katika uchaguzi huu. Kwa
mujibu wa kanuni ya 17 GN. Na 574 wakazi wenye umri wa miaka 21 au zaidi wanaotaka
kugombea nafasi za mwenyekiti wa mtaa, wajumbe za kamati ya mtaa, kundi mchanganyiko
na kundi la wanawake wanahimizwa kuchukua fomu ya kugombea katika ofisi ya
msimamizi msaidizi wa uchaguzi” alisema.
Kuhusu kuchukua
na kurudisah fomu, alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 17 GN. Na. 574 fomu za
kugombea zitatolewa na kutakiwa kurudishwa kuanzia tarehe 1-7 Novemba, 2024 kwa
msimamizi msaidizi wa uchaguzi. “Kwa mujibu wa kanuni ya 17 GN. Na. 574 uteuzi
wa wagombea utafanyika tarehe 8 Novemba, 2024” aliongeza.
MWISHO
Comments
Post a Comment