CCM yaridhishwa na miradi Jiji la Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Chama cha Mapinduzi Mkoa
wa Dodoma kimeridhishwa na utendaji kazi wa serikali baada ya kutembelea na
kukagua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 600,424,100,099
inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Donald Mejiti akiongea wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma
Kauli hiyo ilitolewa na
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Donald Mejiti
alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua
utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma.
Mejiti alisema kuwa kazi
iliyofanyika ni kubwa na nzuri. Alisema kuwa timu yake imetembelea na kukagua
miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 600,424,100,099 na
kujiridhisha kuwa imetekelezwa kwa kiwango bora.
Aidha, alipongeza
ushirikiano baina ya serikali na Chama Cha Mapinduzi kuwa ni mzuri. “Ndugu
zangu tunapopita katika ziara zetu, pia tunaangalia uhusiano baina ya serikali
na chama. Hapa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uhusiano huo ni mzuri na ndiyo
siri ya mafanikio. CCM hakuna sehemu tumeona tunakwamishwa na serikali. Kila
mradi tulioukagua umejengwa vizuri na unavutia” alisema Mejiti.
Wakati huohuo,
aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupunguza migogoro ya Ardhi.
Alisema kuwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa
Wilaya ya Dodoma na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umewezesha
kupunguza migogoro ya Ardhi. “Miongoni mwa ushahidi ni kwamba malalamiko
yanayokuja Ofisi ya CCM Mkoa wa Dodoma yamepungua sana. Ushahidi mwingine ni
juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kulipa fidia wananchi waliokuwa
wakidai” alisema Mejiti.
Katika hatua nyingine
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde aliahidi kuchangia shilingi
milioni 15 ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu na shilingi
milioni tano ununuzi wa viti na meza kwa Shule ya Msingi Iyumbu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akitoa neno la utangulizi |
Kamati ya Siasa ya CCM
Mkoa wa Dodoma ilitembelea mradi wa ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na
matundu 10 ya vyoo Shule ya Sekondari Zuzu, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya
Dodoma, mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje, ujenzi wa Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa Msalato, ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo, mradi wa Maji
Nzuguni na ukarabati wa vyumba 10 vya madarasa Shule ya Msingi Iyumbu.
MWISHO
Comments
Post a Comment