Hospitali ya Wilaya ya Dodoma kuboresha huduma za Afya
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Halmashauri ilianza
ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma kwa lengo la kusogeza huduma za afya
kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Revocatus Baltazary akisoma taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Revocatus Baltazary alipokuwa akisoma
taarifa ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma mbele ya Kamati ya Siasa
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma.
Dkt. Baltazary alisema “kutokana
na changamoto ya kukosa hospitali ya wilaya kwa muda mrefu na changamoto ya
umbali wa kupata huduma za afya kwa ngazi ya wilaya, halmashauri na serikali kuu
iliamua kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma ili kusogeza huduma kwa
wananchi. Hatua hii itawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa ngazi ya wilaya”.
Akiongelea
mapokezi ya fedha, alisema kuwa serikali kuu ilitoa kiasi cha shilingi 1,500,000,000
kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. “Awamu ya kwanza halmashauri ilipokea
kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya maabara, wagonjwa
wa nje, mama na mtoto na kichomea taka. Awamu ya pili halmashauri imepokea
kiasi cha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dawa, mionzi na jengo la kuhifadhia maiti. Hadi hatua
iliyofikia, jumla ya shilingi 1,477,344,488 zimetumika na hivyo, kubakia na
salio la shilingi 22,655,512” alisema Dkt. Baltazary.
Alisema kuwa mradi huo
unatekelezwa kwa muda wa miezi sita kwa utaratibu wa “Force Account” ukisimamiwa
na kamati tatu za ujenzi, manunuzi na mapokezi unatarajiwa kukamilika tarehe 30
Julai, 2024.
Baada ya kukagua ujenzi
wa hospitali hiyo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa,
Donald Mejiti alisema kuwa mradi huo ni mzuri na unaakisi uhalisia na matumizi sahihi
ya fedha. Alisema kuwa hospitali hiyo imejengwa eneo la kimkakati kwa sababu
eneo la Nala ni kitovu cha viwanda katika jiji hilo.
Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ni moja kati ya halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma, ina jumla ya Vituo 45
vya kutolea huduma, kati hivyo, vituo 38 ni zahanati na sita ni vituo vya afya.
Idadi kubwa ya wananchi wanapata huduma za afya ngazi ya wilaya katika
Hospitali ya Mtakatifu Gemma iliyopo Kata ya Miyuji.
MWISHO
Comments
Post a Comment