RC Senyamule aagiza utengenezaji Viti uende sambamba na ujenzi wa madarasa Sekondari Mtumba
Na. Dennis Gondwe, MTUMBA
MKUU
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameagiza ujenzi wa madarasa uende
sambamba ya utengenezaji wa viti na meza kwa ajili ya wanafunzi ili vyote
vikamilike pamoja na kuanza kutoa huduma.
Kauli
hiyo aliitoa alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa nane na
matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Mtumba iliyopo Kata ya Mtumba, Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
Baada
ya kukagua hatua ya ujenzi wa miundombinu hiyo alihoji hatua ya utengenezaji wa
viti na meza ambao ulikuwa haujaanza. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliagiza utaratibu
wa kutengeneza viti na meza uanze ili uende sambamba ya ujenzi wa miundombinu
hiyo na kukamilika pamoja ili isicheleweshe utoaji wa huduma.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa madarasa nane na matundu 10 ya vyoo kwa ajili ya mapokezi
ya wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2024/2025 Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtumba,
Mwl. Stephen Moshi alisema kuwa ujenzi unaendelea vizuri. “Shule ilipokea
shilingi 201,000,000 tarehe 6 Januari, 2024 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa
nane na matundu 10 ya vyoo. Kwa upande wa vyumba nane vya madarasa umekamilika
kwa asilimia 100 na ujenzi wa matundu ya vyoo upo hatua ya umaliziaji sawa na
asilimia 75” alisema Mwl. Moshi.
Akiongelea
faida za mradi huo alizitaja kuwa ni kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha tano
kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kupata elimu hiyo kutokana na kujengewa
miundombinu wezeshi ya kufundishia na kujifunzia. Faida nyingine ni ajira wa
wananchi wanaozunguka shule hiyo kutokana na shughuli mbalimbali zitakazokuwa
zinafanyika.
Shule
ya Sekondari Mtumba ipo katika Kata ya Mtumba umbali wa kilometa 23 kutoka
katikati ya Jiji la Dodoma ikihudumia wanafunzi 641 wakidato cha kwanza hadi
cha nne kutoka mitaa ya Majengo, Mtumba na Vikonje na baadhi ya wanafunzi
kutoka Mahoma Makulu na Ipala.
MWISHO
Comments
Post a Comment