RC Dodoma afurahishwa ujenzi Sekondari Mtemi Chiloloma
Na. Dennis Gondwe, HOMBOLO MAKULU
MKUU
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameagiza ujenzi wa Shule ya Sekondari Mtemi
Chiloloma kusimamiwa vizuri ili ukamilike katika muda uliopangwa kwa ajili ya
kutoa huduma.
Agizo
hilo alilitoa alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa
shule hiyo iliyopo katika Kata ya Hombolo Makulu, jijini Dodoma.
Awali
akikagua ujenzi huo alieleza kufurahishwa kwake na hatua ya ujenzi wa shule
hiyo. Aliwataka viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusimamia vizuri
mradi huo ili uweze kukamilika katika muda uliopangwa.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 18 ya vyoo kwa Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma, Mwl. Livinus Tanganyika
alisema shule yake ilipokea shilingi 216,000,000 kutoka serikali kuu. “Ujenzi
ulianza tarehe 25 Novemba, 2023 mpaka sasa ujenzi wa madarasa umekamilika kwa
asilimia 100, matundu ya vyoo 18 yapo hatua ya umaliziaji, kazi inayoendelea ni
kuweka marumaru. Mradi unategemea kukamilika kabla au ifikapo tarehe 10 Mei, 2024”
alisema Mwl. Tanganyika.
Akiongelea
faida za mradi huo, alisema kuwa utakapokamilika utaongeza ufaulu wa wanafunzi
kwa sababu mazingira ya kufundishia na kujifunzia yatakuwa yameboreshwa. Faida nyingine
aliitaja kuwa mradi unatoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo kuanzia kwa
mafundi na wasaidizi wao.
Kwa
upande wa mwananchi mkazi wa Hombolo, Jeremiah Samwel alisema kuwa kitendo cha
serikali kujenga shule hiyo mpya kinaonesha dhamira ya serikali katika kujali
elimu ya wananchi wake. Shule hii inawasaidia sana wananchi wa maeneo haya kwa
sababu isingejengwa wanafunzi wangekosa fursa ya elimu, aliongeza.
Shule
ya Sekondari Mtemi Chiloloma ipo umbali wa kilometa 54 kutoka katikati ya Jiji
la Dodoma ikihudumia wanafunzi kutoka mitaa ya Zapisa, Msisi, Mayeto, Tandahima
na Masea ikiwa na idadi ya wanafunzi wa kidato cha hadi cha nne 527 na walimu
10.
MWISHO
Comments
Post a Comment