Mchengerwa: ALAT simamieni nidhamu ya Madiwani na Wakurugenzi
OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kushuka kwa nidhamu ya baadhi ya
madiwani na wakurugenzi ni matokeo ya kulegalega kwa utendaji kazi wa Jumuiya
ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).
Waziri Mchengerwa amesema jukumu la msingi la (ALAT) ni
kuimarisha nidhamu na ushirikiano baina ya baraza la madiwani na watendaji wa
serikali kuhakikisha wanaongea lugha moja katika kuwahudumia wananchi na
kuwaletea maendeleo.
Amesema “Msingi wa uanzishwaji wa (ALAT) mwaka 1984, baba wa
taifa Julius Kambarage Nyerere alikusudia mengi ambayo kama (ALAT) wakifanya
vizuri leo, wataweza kutusaidia kuyaboresha na kutuweka sawa”
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo katika kikao kazi kilicho
wakutanisha wajumbe wa kamati tendaji ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) na viongozi wa juu wa OR – TAMISEMI na PPRA kilicholenga kujadiliana
namna bora ya kuboresha utendaji kazi wa jumuiya hiyo.
Akizungumzia madai ya uwepo wa baadhi ya mifumo inayokwamisha
manunuzi, Waziri Mchengerwa amesema wakati mwingine viongozi wa ngazi za juu
wamekuwa wakichukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi hasa wakurugenzi kwa
madai ya kuchelewesha manunuzi ilihali wakati mwingine wakurugenzi
wakikwamishwa na mifumo.
“Tumejikuta tunalazimika kuwaadhibu wakurugenzi, kumbe wakati
mwingine makosa siyo yao ni ya mifumo ya manunuzi au pengine ni mipya kwao ama
hawana elimu au uelewa wa kutosha kuhusiana na mifumo hiyo” alisema Waziri
Mchengerwa
Ili kupata utatuzi wa hoja hizo za kimsingi zinazodaiwa
kukwamisha utendaji kazi wa baadhi ya halmashauri, waziri Mchengerwa alimpa
fursa afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA Bw.
Eliakim Maswi kutoa ufafanuzi wa kina na elimu juu ya namna mifumo ya manunuzi
inayotumiwa na serikali inavyopaswa kufanya kazi.
Akiongea kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo mwenyekiti wa ALAT
Taifa Mhe. Murshid Ngeze, amepongeza hatua ya kukutanishwa na watendaji wa juu
wa OR – TAMISEMI na PPRA na kusema kuwa wamefarijika kukutanishwa na viongozi
hao na kikao hicho ni mwanzo wa kwenda kuonesha uimara wa serikali za
mitaa na kuondoa kero ndogondogo ambazo zinamchukiza Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu.
Comments
Post a Comment